MAKAMU WA RAIS AAGIZA OPERESHENI MAALUMU TUNDURU KUKABILI WACHOCHEZI WA MIGOGORO YA WAKULIMA NA WAFUGAJI
Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameagiza kuanza mara moja kwa operesheni
maalumu ya kuwabaini na kuwakamata watu wanaochochea migogoro ya wakulima na
wafugaji katika Wilaya ya Tunduru, Mkoa wa Ruvuma, huku akitaka kupatiwa
taarifa ya hatua zilizochukuliwa akiwa bado katika ziara yake mkoani humo.
Akizungumza katika
mkutano wa hadhara na wananchi wa Tunduru, Makamu wa Rais amesema Serikali ya
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imesikia kilio cha wananchi kutokana na migogoro
hiyo iliyosababisha vifo vya watu, wakiwemo wananchi, viongozi na askari, na
kwamba wakati umefika wa kuchukua hatua madhubuti kurejesha amani.
Ameelekeza Mkuu wa
Mkoa wa Ruvuma, Mkuu wa Wilaya ya Tunduru na Kamati za Ulinzi na Usalama
kuwachukulia hatua wote watakaobainika kuchochea migogoro hiyo, bila kujali
nafasi zao, nyadhifa au itikadi zao za kisiasa.
Makamu wa Rais
amesema baadhi ya viongozi wa vijiji wanadaiwa kushiriki katika uuzaji wa
maeneo na kuwaingiza wafugaji katika maeneo yasiyoruhusiwa, hali inayochangia
migogoro ya mara kwa mara kati ya wakulima na wafugaji.
Amesisitiza kuwa
matumizi ya ardhi ya vijiji lazima yazingatie sheria na ushirikishwaji wa
wananchi badala ya maamuzi ya watu wachache wenye maslahi binafsi.
Aidha, ameeleza
kuwa Serikali inaendelea kutafuta suluhu ya kudumu kupitia timu ya kitaifa na
wizara zinazohusika, lakini juhudi hizo zinapaswa kwenda sambamba na hatua za
haraka dhidi ya wanaochochea migogoro.
Kwa upande wake,
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Mahmoud amesema Serikali imepokea
maelekezo hayo na kwamba Jeshi la Polisi litashirikiana na mamlaka nyingine
kuhakikisha wote wanaobainika kuhusika wanachukuliwa hatua kwa mujibu wa
sheria.
Amesema takribani
watu 12 wamepoteza maisha kutokana na migogoro hiyo, huku zaidi ya vikosi 20
vya askari vikiendelea na operesheni ya kuwaondoa wafugaji wanaofuga katika
maeneo yasiyoruhusiwa kwa mujibu wa mipango ya matumizi bora ya ardhi.
Katika hatua
nyingine, Makamu wa Rais ameagiza kuimarishwa kwa usimamizi wa mradi wa ujenzi
wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovolti 220 kutoka
Songea–Tunduru–Masasi–Mahumbika, akielekeza kubadilishwa kwa meneja wa mradi
kutokana na kutoridhishwa na kasi ya utekelezaji wake.
Amesema Serikali
tayari imetoa zaidi ya shilingi bilioni 42 kwa mkandarasi, hivyo hakuna sababu
ya mradi huo kuendelea kusuasua wakati wananchi wa Tunduru na mikoa ya Lindi na
Mtwara wanahitaji umeme wa uhakika kwa ajili ya shughuli za kiuchumi.
Kuhusu maendeleo
ya Wilaya ya Tunduru, Makamu wa Rais ameelekeza kufuatiliwa kwa ombi la ujenzi
wa soko la kisasa, ambapo Waziri mwenye dhamana ya TAMISEMI amesema maandalizi
ya mradi huo yamefikia hatua ya kuwasilishwa kwa andiko katika Tume ya Mipango,
huku Serikali ikitarajia kuanza ujenzi katika mwaka wa fedha 2027/2028.
Waziri huyo pia
amesema taratibu za kushughulikia ombi la kuigawa Halmashauri ya Wilaya ya
Tunduru ili kuanzisha halmashauri mbili zinaendelea, baada ya tathmini ya awali
kufanyika.
Makamu wa Rais
amehitimisha ziara yake mkoani Ruvuma kwa kuwahakikishia wananchi wa
Ruvuma kuwa Serikali itaendelea
kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo sambamba na kuhakikisha amani na
usalama vinarejea, ili wananchi waweze kufanya shughuli zao za kiuchumi bila
hofu.

Post a Comment