Katibu wa Bunge Awataka Wabunge wa Bunge la Vijana 2026 Kuzingatia Nidhamu, Haki na Uwajibikaji
Na Mwandishi Wetu
Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Baraka Leonard, amewataka Wabunge wa Bunge la Vijana 2026 kuzingatia misingi ya demokrasia, haki, nidhamu na uwajibikaji katika kutekeleza majukumu yao, huku wakiheshimu mitazamo tofauti na kufuata Kanuni na taratibu za Kibunge.
Akizungumza leo Novemba 10, 2026 jijini Dodoma wakati wa ufunguzi rasmi wa Bunge hilo la siku tano lililoanza Novemba 9 na kutarajiwa kuhitimishwa Novemba 13, 2026, Leonard amesema jukwaa hilo linawaandaa vijana kuwa viongozi bora wa sasa na baadaye kwa kuwapa mafunzo kuhusu historia ya Bunge, uendeshaji wa shughuli za Kibunge, taratibu za kutunga sheria, na Kanuni za Bunge hilo.
Katika hatua za awali, washiriki hao tayari wamepata uzoefu wa vitendo wa mifumo ya kidemokrasia kwa kufanya uchaguzi wa Spika, Naibu Spika, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Walio Wachache, Katibu wa Bunge na Makatibu Mezani, sambamba na kushiriki mchakato wa kuthibitisha jina la Waziri Mkuu na uteuzi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Leonard amewapongeza viongozi waliochaguliwa na kuwataka kuongoza kwa haki, usawa na busara bila upendeleo, huku akiwahimiza ambao hawakupata nafasi za uongozi kuendelea kuchangia mijadala yenye tija, akisisitiza kuwa uongozi si kushika nafasi pekee bali ni dhamana inayopimwa kwa mchango, uwajibikaji na matokeo kwa jamii.
Aidha, Katibu wa Bunge amewahimiza vijana hao kulitumia Bunge hilo si tu kuibua changamoto za vijana katika sekta za elimu, ajira, ujasiriamali, teknolojia, afya, mazingira, ushiriki wa maamuzi na fursa za kiuchumi, bali pia kuchambua vyanzo vyake na kupendekeza suluhisho zinazotekelezeka.
Amesema mafanikio ya Bunge hilo yatajengwa juu ya misingi minne mikuu ambayo ni nidhamu na uzingatiaji wa Kanuni, uwezo wa kujenga hoja zenye ukweli, ushahidi na mantiki kwa weledi, uwajibikaji katika uwakilishi, pamoja na uadilifu, uzalendo na dhamira ya kulitumikia Taifa, akibainisha kuwa uwezo wa kiongozi hupimwa kwa kusikiliza na kujibu hoja kwa busara badala ya wingi wa maneno.
Akizungumzia historia ya chombo hicho, Leonard ameeleza kuwa vijana hao watapata fursa ya kipekee ya kujadili na kupitisha Muswada wa Sheria wa Maadhimisho ya Miaka 100 ya Bunge la Tanzania tangu kuanzishwa kwa Baraza la Kutunga Sheria la Tanganyika (The Legislative Council of Tanganyika Territory) mwaka 1926.
Maadhimisho hayo ya mwaka 2026 yenye kaulimbiu isemayo "Miaka 100 ya Bunge: Historia Yetu, Dira Yetu," yanalenga kutafakari safari ya Bunge na kuhifadhi historia, nyaraka, misingi na tunu za Kibunge ili virithishwe kwa vizazi vijavyo.
Kwa upande wake, Spika wa Bunge la Vijana 2026, Anna Mrema, amewataka vijana kutambua wajibu wao wa kuleta mabadiliko chanya kwa kuanza kuchukua hatua sasa badala ya kusubiri nafasi za uongozi baadaye au kuishia kulaumu viongozi. Amesema uongozi ni dhamana na huduma kwa watu na si nafasi ya kujinufaisha binafsi, hivyo amewataka washiriki hao kuzingatia nidhamu, uadilifu na heshima, na kuwa mabalozi wa mabadiliko watakaporejea vyuoni na katika jamii zao kwa kusambaza maarifa waliyoyapata.
Post a Comment