NDEJEMBI AHOJI VIONGOZI KUTOTEKELEZA AGIZO LA RAIS




Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, amehitimisha ziara yake wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma kwa kutatua migogoro mikubwa mitatu inayowakabili wakulima na kuagiza hatua za haraka za kisheria na kinidhamu dhidi ya viongozi na kampuni zinazozorotesha sekta ya kilimo. 

Katika suala la ardhi, Makamu wa Rais ameihoji na kuibana Wizara ya Kilimo pamoja na Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) kwa kuchelewesha utekelezaji wa agizo la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan lililotolewa Februari 2024 la kurejesha nusu ya shamba la ekari 6,500 kwa wananchi. 

Baada ya kubaini mkanganyiko wa taarifa kati ya viongozi wa ASA waliodai kutoa maeneo na madiwani waliothibitisha wananchi kutopata ardhi hiyo, Mhe. Ndejembi ametaka apewe maelezo ya haraka kabla ya siku kuisha kuhusu mahali zilipo takribani ekari 2,100 na kuonya kuwa Serikali haitasita kuwawajibisha watendaji wanaokwamisha maelekezo ya Mkuu wa Nchi.

Katika hatua nyingine ya kukabiliana na kero za kiuchumi za wakulima, Mhe. Ndejembi ameingilia kati sakata la madeni ya wakulima wa tumbaku wa Kata ya Mgombasi wanaoidai kampuni ya Three H na vyama vya ushirika takribani dola za Marekani 849,000 kutoka msimu uliopita.

 Makamu wa Rais ameagiza pande zote mbili kusaini makubaliano ya maandishi mbele ya Mkuu wa Wilaya ili kukamilisha malipo hayo kabla ya mwisho wa mwezi huu, akielekeza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuwasaka na kuwachukulia hatua za kisheria wote watakaokiuka makubaliano hayo.

 Sambamba na hilo, ametatua kero ya soko la mahindi kwa kumwagiza Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Dkt. Komba, kuanza mara moja ununuzi wa mahindi mkoani humo kwa bei mpya ya shilingi 500 kwa kilo iliyoelekezwa na Rais Samia, huku akionya vikali dhidi ya watumishi wowote wanaopanga kuwadhulumu wakulima .

No comments