Mbunifu wa mavazi anasuliwa kwenye ukahaba wa lazima


 


Shirika la Global Anti-Human Trafficking Organisation (GAHTO) na wakala wa serikali wa Nigeria wa kupambana na biashara haramu ya binadamu, NAPTIP, wamefanikiwa kuwaokoa wanawake wawili kutoka kwenye mtego wa kutumikishwa kingono nchini Mali.

Mmoja wa mabinti hao ni mbunifu wa mavazi mwenye umri wa miaka 24, Joy, aliyekuwa akiishi Port Harcourt katika jimbo la Rivers nchini Nigeria.

 Joy alirubuniwa na jirani aliyemchukulia kama rafiki kwa ahadi ya kazi ya ubunifu wa mitindo na duka la nguo nchini Mali ili aweze kuweka akiba ya kuanzisha biashara yake.

Hata hivyo alipofika nchini humo, alikuta mazingira ya ukahaba na alipokataa kujiingiza kwenye biashara ya ngono alikumbana na vipigo, udhalilishaji na vitisho kabla ya kufanikiwa kutoroka.

Uokoaji huu uliofanyika wiki iliyopita unaonyesha ukatili wa mitandao ya usafirishaji haramu wa binadamu inayotumia ahadi za uongo za ajira, umaskini na imani kwa watu wa karibu kuwanasa wanawake na wasichana.

Mbali na Joy, mwathirika mwingine ni msichana wa miaka 16 kutoka jimbo la Delta ambaye alikuwa ameacha shule na kushawishiwa na mwanamke wa jamii yake kwa ahadi ya kazi ya biashara nje ya nchi.

Msichana huyo alilazimishwa kufanya biashara ya ngono kwa wiki tatu mfululizo huku akitishiwa kupigwa na kupigwa sindano bila maelezo ya wazi ni ya nini kabla ya kutoroka kwa msaada wa msamaria mwema, na kwa sasa yuko chini ya uangalizi wa ofisi ya kanda ya Benin ya NAPTIP.

Mwanzilishi wa GAHTO, Prosper Michael, ameeleza kuwa visa hivyo ni sehemu ya mwenendo mpana wa raia wa Nigeria, hususan wanawake na wasichana vijana, wanaovushwa mipaka ya Afrika Magharibi kwa udanganyifu wa ajira na kukumbana na utumikishwaji kingono.

Amesisitiza kuwa kuwarejesha wahanga Nigeria pekee hakutoshi bila kuwawezesha na kukabiliana na vyanzo vya tatizo ikiwemo ukosefu wa fursa, mifumo dhaifu ya hifadhi ya kijamii na ukosefu wa usawa wa kijinsia.

Amewataka viongozi na wake wa magavana wa majimbo, hasa wa jimbo la Delta, kuunga mkono programu za uwezeshaji kiuchumi na kumsaidia msichana huyo wa miaka 16 kurejea shuleni ili kuzuia madhara zaidi ya janga lililomkumba.

No comments