SERIKALI KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA BODABODA KUIMARISHA UTULIVU NA KUKUZA UCHUMI



Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amesema kuwa Mkoa wa Dar es Salaam utaendelea kushirikiana kwa karibu na makundi ya waendesha bodaboda, bajaji, machinga, mama lishe na baba lishe kwa lengo la kuimarisha uchumi na kudumisha amani na utulivu nchini. 

Akizungumza leo Jumapili Julai 5, 2026 katika mkutano uliowakutanisha viongozi wa makundi hayo na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, Mpogolo amebainisha kuwa makundi haya ni nguzo muhimu ya uchumi wa Tanzania kwa kuwa yanatoa ajira kwa maelfu ya vijana na kusaidia ustawi wa familia nyingi, ambapo sasa yamepata heshima na fursa ya kushirikishwa katika maamuzi kutokana na falsafa ya Rais Samia Suluhu Hassan ya maridhiano, mageuzi, ujenzi mpya na utu.

Ili kuunga mkono juhudi hizo na kuhakikisha utulivu unadumu wakati wote wa shughuli zao za kila siku, Mpogolo amesisitiza umuhimu wa kuimarishwa kwa ushirikiano wa karibu kati ya Jeshi la Polisi, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) na viongozi wa bodaboda.

Amesema hatua hiyo itasaidia kuongeza elimu ya usalama barabarani, kuimarisha uzingatiaji wa sheria na kulinda usalama wa watumiaji wote wa barabara, jambo linaloenda sambamba na jitihada za Serikali za kutenga fedha za mikopo kupitia halmashauri na kujenga masoko ili kuboresha mazingira ya wafanyabiashara wadogo nchini.

Ushirikiano huu unakuja wakati ambapo vyombo vikuu vya ulinzi nchini vikiwemo Jeshi la Polisi na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kupitia taarifa zao zilizotolewa hivi karibuni  vimesisitiza umuhimu wa wananchi kudumisha amani na kuepuka vishawishi vya kuvunja sheria. 

Vyombo hivyo vimebainisha kuwa viko imara na vinaendelea kushirikiana ili kuhakikisha amani na utulivu vinakuwepo wakati wote, hasa kuelekea maadhimisho ya Sikukuu ya Sabasaba na Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa, hivyo kuwataka wananchi na makundi yote ya kiuchumi kuendelea na shughuli zao bila hofu yoyote.  

No comments