Madereva wa Kitanzania nchini Qatar wateta na Waziri wa Nchi, Sangu
Madereva wa Kitanzania nchini Qatar wameteta na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, ambaye amewahimiza kuzingatia nidhamu, uwajibikaji na uadilifu wanapotekeleza majukumu yao.
Katika mazungumzo yaliyofanyika Julai 8,2026 jijini Doha, Waziri Sangu alisisitiza kuwa tabia njema na weledi wa wafanyakazi hao wanaohudumu katika kampuni ya MOWASALAT ni nguzo muhimu inayojenga taswira nzuri ya Tanzania na kufungua milango ya ajira kwa vijana wengi zaidi nyumbani.
Amesema kuwa mafanikio yanayoendelea kupatikana kwa Watanzania katika nchi mbalimbali yanatokana na juhudi, kujituma na kuonesha uwezo katika maeneo yao ya kazi.
“Uwepo wa Watanzania wanaofanya kazi katika mataifa ya nje kwa bidii ni sifa kubwa kwa taifa, kwani inasaidia kujenga imani na mahusiano mazuri kati ya Tanzania na mataifa mengine, hivyo kutoa fursa zaidi kwa vijana wengine kupata nafasi za ajira na kujifunza,” amesema Waziri Sangu.
Alibainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kupambana kuweka mazingira wezeshi na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa ili kuongeza fursa hizo za ajira nje ya nchi.
Waziri Sangu aliwataka madereva hao kuendelea kushirikiana kwa karibu na Ubalozi wa Tanzania nchini humo ili kupata miongozo ya kisheria, huku akiwasihi kuwa mabalozi wema na kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi Jamii (NSSF) kupitia Hifadhi Scheme kwa ajili ya usalama wa kipato chao cha baadaye.
Akizungumzia mkutano huo, Balozi wa Tanzania nchini Qatar, Mhe. Habibu Awesi Mohamed, aliwahakikishia madereva hao kuwa ubalozi utakuwa tayari kuwapa ushirikiano na msaada wa kisheria wakati wowote.
Kwa upande wa Madereva hao wakizungumza kwa nyakati tofauti, wameshukuru Serikali kwa kuwaunganisha na fursa za ajira nje ya nchi.
“Tunaishukuru sana Serikali kwa kutufungulia milango ya ajira nje ya nchi. Tunaomba juhudi hizi ziendelezwe ili vijana wengi zaidi waliopo Tanzania wapate fursa kama tulizopata sisi kwa kuwa zitaboresha maisha yao pamoja na kuwawezesha kuchangia maendeleo ya Taifa,” amesema Zulekifli Ali Massawe








Post a Comment