BALOZI YAKUBU NA TFB WAWEKA MIKAKATI YA KUKUZA SEKTA YA FILAMU TANZANIA KUPITIA USHIRIKIANO NA UFARANSA
Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Mheshimiwa Balozi Saidi Othman Yakubu, amekutana na Dkt. Gervas Kasiga, Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania (TFB), katika Ubalozi wa Tanzania mjini Paris kwa mazungumzo yaliyolenga kuweka mikakati ya kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Ufaransa katika sekta ya filamu.
Mazungumzo hayo yalijikita katika fursa za kubadilishana uzoefu, kukuza uwekezaji katika tasnia ya filamu, pamoja na kuanzisha ushirikiano rasmi kati ya Bodi ya Filamu Tanzania na taasisi mbalimbali za filamu nchini Ufaransa.
Aidha, viongozi hao walijadili namna ya kuwezesha ushiriki wa TFB na wadau wake katika matamasha na maonesho mbalimbali ya filamu yanayofanyika Ufaransa na Tanzania, kwa lengo la kuitangaza Tanzania kama kitovu cha utengenezaji wa filamu na maudhui ya ubunifu barani Afrika.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Balozi Yakubu alisisitiza kuwa Ubalozi utaendelea kuwa daraja la kuunganisha wadau wa sekta ya ubunifu kutoka Tanzania na Ufaransa ili kuimarisha ushirikiano, kuvutia uwekezaji na kufungua masoko mapya kwa watayarishaji wa filamu wa Tanzania.
Kwa upande wake, Dkt. Kasiga alieleza dhamira ya Bodi ya Filamu Tanzania ya kupanua ushirikiano wa kimataifa ili kuinua ubora, ushindani na mchango wa sekta ya filamu katika uchumi wa Taifa kupitia ubia wa kimkakati na taasisi za kimataifa.
Alibainisha kuwa ushirikiano huo utafungua fursa mpya za mafunzo, ubadilishanaji wa teknolojia, uzalishaji wa pamoja wa filamu na ushiriki mpana zaidi wa wadau wa filamu wa Tanzania katika majukwaa ya kimataifa.



Post a Comment