KHANGA YATIKISA PARIS
Paris iligeuka kuwa jukwaa la tamaduni za Afrika Mashariki huku vazi la khanga likiteka hisia za dunia chini ya mwanga wa Mnara wa Eiffel na kandokando ya Mto Seine.
Hayo yametokea wakati wa kuadhimisha Siku ya Kiswahili Duniani mwaka 2026, tamasha maarufu la ‘Usiku wa Mswahili’ lililotimua vumbi ndani ya kumbi za Makao Makuu ya UNESCO, likishuhudia wabunifu nguli wa Kitanzania wakichora taswira ya urithi wa taifa kwa kutumia vitambaa vyenye ujumbe mwanana.
Tukio hili likiwa ni sehemu ya Kongamano la Pili la Kimataifa la Kiswahili na Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani (MASIKIDU), halikurusha tu maneno ya lugha hiyo adhimu, bali lilivika Paris vazi la heshima na madoido ya kitamaduni.
Wakati mbunifu Mustafa Hassanali akizindua ubunifu wake ulioshonwa kwa chapa halisi ya Kiswahili, mwanamitindo mashuhuri Miriam Odemba aliteka nyoyo za wageni wa kimataifa akitandaza jukwaani ubunifu wa khanga kutoka kwa Fiderine Iranga.
Hali ilizidi kuwa ya msisimko pale Joyce Sianga wa ‘Jojo African Design’ alipomwaga mitindo mchanganyiko ya khanga iliyothibitisha kuwa vazi hilo linaweza kuzungumza lugha yoyote ya mitindo duniani.
Kama hiyo haikutosha, Miss World Tanzania 2026, Latricia Ian, alikamilisha simulizi hiyo ya uzuri wa Kiafrika kwa kutokeza akiwa ametinga gauni maridadi la khanga lililobeba utambulisho mzito wa Tanzania na kuacha gumzo kubwa jijini Paris.

Post a Comment