Azam Amputee Football 2026): Vigogo waanza kwa kishindo
Michuano ya Ligi Kuu ya Soka la Watu Wenye Ulemavu (Azam Amputee Football 2026) imeanza kwa kasi ya ajabu katika Uwanja wa KMC Complex jijini Dar es Salaam, huku timu za L.S.L, Black Eagle Academy na Duce Parasport zikionyesha ubabe mkubwa tangu siku ya kwanza ya mashindano hayo.
Katika michezo iliyojaa burudani na ushindani, L.S.L iliibuka na ushindi mnono wa mabao 10-0 dhidi ya Lango la SADC, huku ikionyesha makali yake kwa kuicharaza pia Songwe mabao 11-0.
Kwa upande wake, Black Eagle Academy haikuwa nyuma, ikiifunga Unyanyembe Amputee mabao 9-0 kabla ya kuichapa Zanzibar Combine mabao 6-2, wakati Duce Parasport ikianza vyema kwa kuicharaza Songwe mabao 6-0 na kuifunga Lango la SADC mabao 3-0.
Michezo mingine ilitoa upinzani mkali ambapo Zanzibar Combine iliibuka na ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Arusha Warriors, huku Sauti Parasport ikipata ushindi wa 2-1 dhidi ya Duce Parasport. Nayo Njombe Warriors iliifunga Arusha Warriors bao 1-0 katika pambano lililokuwa na ushindani mkubwa.
Akizungumzia mwelekeo wa mashindano hayo, Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TAFF), Shaban Msangi, amesema kuwa ligi hiyo inayozikutanisha klabu 10 kutoka Tanzania Bara na timu moja kutoka Zanzibar ni hatua muhimu katika kukuza mchezo huo.
Msangi amesisitiza kuwa ligi hii inatoa jukwaa adhimu la kuibua vipaji vipya na kukiendeleza soka la watu wenye ulemavu nchini ili liweze kufikia viwango vya kimataifa.

Post a Comment