Aston Villa yaingia mkataba mnono na Visit Rwanda
![]() |
| Rais wa Shughuli za Biashara wa Aston Villa, Francesco Calvo, na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya RCB, Janet Karemera, wakizindua rasmi ushirikiano kati ya Visit Rwanda na Aston Villa nchini Uingereza. |
Klabu ya Aston Villa inayoshiriki Ligi Kuu nchini England imeingia mkataba mnono wa ushirikiano na bodi ya utalii ya Rwanda, Visit Rwanda, ambao sasa itakuwa mdhamini mkuu wa jezi za timu hiyo.
Kupitia makubaliano hayo, nembo ya Visit Rwanda itaonekana kifuani mwa jezi za timu ya wanaume, wanawake, pamoja na timu za vijana za akademi ya klabu hiyo, huku ikiwa ni mbadala wa kampuni ya kamari ya Betano iliyokuwa ikidhamini jezi hizo hapo awali.
Ushirikiano huu unaifanya Aston Villa kuwa klabu ya pili nchini Uingereza kufanya kazi na Visit Rwanda baada ya Arsenal, ambayo ilihitimisha ushirikiano wake wa miaka minane na nchi hiyo mnamo Juni 30.
Rais wa Shughuli za Biashara wa Aston Villa, Francesco Calvo, ameeleza kuwa huu ni mwanzo wa kusisimua kwa klabu hiyo katika kupanua wigo wake wa kimataifa, akisisitiza kuwa wanatarajia kunufaika kupitia fursa mbalimbali za uwekezaji, utalii, na maendeleo ya michezo.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya RCB, Janet Karemera, amesema kuwa hatua hiyo ni mwendelezo wa mikakati ya Rwanda ya kuitangaza nchi hiyo kama kitovu cha utalii na biashara nchini Uingereza, ambayo ni miongoni mwa masoko muhimu kwa taifa hilo.
Ameongeza kuwa ushirikiano huu utasaidia kutanua wigo wa utambulisho wa Rwanda kwa hadhira ya kimataifa, huku wakilenga pia kukuza vipaji vya soka na kubadilishana ujuzi kupitia programu za mafunzo ya ukocha na miradi ya kijamii.
Mbali na kuonekana kwenye jezi, makubaliano hayo yatajikita katika kukuza Rwanda kama eneo bora la uwekezaji, mikutano ya kimataifa, na matukio makubwa ya michezo.
Pande zote mbili zinatarajia kushirikiana katika mipango mbalimbali ya maendeleo ya soka, uongozi, na kusaidia ukuaji wa mazingira ya mpira wa miguu nchini Rwanda, huku wakijenga daraja imara la uhusiano kati ya klabu hiyo ya kihistoria na taifa hilo la Afrika Mashariki.

Post a Comment