Msangi apongeza Mwitikio wa mikoa soka kwa walemavu


Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu kwa Watu Wenye Ulemavu Tanzania (TAFF), Shabani Msangi, amepongeza mikoa iliyojitokeza kushiriki msimu wa tatu wa mashindano ya Azam Amputee Football Tournament (AAFT) 2026, akisisitiza kuwa mwitikio huo ni kielelezo tosha cha ukuaji na maendeleo ya kasi ya mchezo huo nchini. 

Msangi amebainisha kuwa ongezeko la timu zinazoshiriki ni ishara ya mafanikio makubwa kwa kuwa linatoa fursa pana kwa wachezaji wenye ulemavu kuonyesha vipaji vyao na kuongeza ushindani uwanjani. 

Shirikisho hilo linaendelea kuhamasisha mikoa mingine kujitokeza katika misimu ijayo ili kuimarisha kiwango cha mchezo na kupanua wigo wa ushiriki kwa ajili ya maendeleo ya mpira wa miguu kwa watu wenye ulemavu nchini.

Katika muktadha huo wa maendeleo, Katibu Mkuu wa TAFF, Alfred Sentau, amesisitiza kuwa mpira wa miguu kwa watu wenye ulemavu umeendelea kuwa chachu ya matumaini kwa kuwapa wachezaji fursa ya kudhihirisha kuwa ulemavu si kikwazo cha kufikia ndoto zao.

Sentau amesema kuwa mashindano yanayoendelea katika Uwanja wa KMC Complex Mwenge yamefuta dhana potofu ya jamii inayochukulia ulemavu kama kutoweza, badala yake yameonyesha kuwa watu hawa wana uwezo mkubwa wa kushindana na kufanya makubwa kama watu wengine. 

Amekumbushia kuwa wakati ligi hiyo inaanzishwa ilikuwa na vilabu vinne pekee, lakini sasa imekua na kufikia vilabu kumi, jambo linaloashiria mageuzi makubwa katika sekta hiyo.

Lengo kuu la TAFF kwa sasa ni kuendelea kuiboresha ligi hiyo ili kuzalisha wachezaji bora watakaounda Timu ya Taifa imara yenye uwezo wa kushindana katika medani za kimataifa. 

Kufuatia kuanza rasmi kwa mashindano hayo tarehe 13 Julai 2026, Sentau ametoa wito kwa wadau mbalimbali kujitokeza kuunga mkono na kuwezesha maendeleo ya mchezo huo. 

Amesema kuwa uwekezaji katika soka la walemavu utawasaidia wachezaji kujitegemea kiuchumi na kuendelea kujenga taifa lenye usawa, ujumuishi na fursa sawa kwa wananchi wote kupitia michezo. 

No comments