Watanzania Watakiwa Kuachana na Taarifa Zisizo Sahihi za Mitandao ya Kijamii Kuhusu Ubia wa Tanzania na EU
Serikali
imewataka wananchi kuachana na taarifa zisizo sahihi zinazosambazwa kwenye
mitandao ya kijamii na baadhi ya vyombo vya habari ambazo zinapotosha ukweli
kuhusu kura iliyopigwa na Bunge la Ulaya.
Kupitia taarifa
ya Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, imesisitizwa kuwa kura hiyo iliyopigwa
Juni 18, 2026, kuhusu Mpango wa Ushirikiano kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya
(EU) kwa mwaka 2026 si uamuzi wa mwisho wa EU kuhusu programu hiyo yenye
thamani ya Euro milioni 156.
Serikali imebainisha
kuwa hatua hiyo ni sehemu tu ya mchakato wa ndani wa taasisi za EU ambapo Bunge
limetoa maoni na mapendekezo kwa mamlaka nyingine zinazohusika na maamuzi ya
mwisho, na sio tamko la kusitisha ushirikiano.
Kinyume
na upotoshaji unaoenea mitandaoni, mapendekezo yaliyotolewa na Bunge la Ulaya
hayahusu kusimamishwa kwa fedha za programu zinazotekelezwa au zinazotarajiwa
kutekelezwa nchini, bali yanahusu kufanyiwa mapitio kwa programu hiyo na
kuwasilishwa tena.
Serikali
imefafanua kuwa mapitio yoyote ya programu ya ubia hufanyika kwa njia ya
mashauriano na makubaliano ya pande zote mbili na hatimaye kuridhiwa kupitia
Mkataba wa Pamoja wa Fedha.
Aidha, imeelezwa
kuwa kati ya Euro milioni 156 zilizotengwa, Euro milioni 17 pekee ndizo
zilizopangwa kupitia moja kwa moja katika mifumo rasmi ya Serikali, huku kiasi
kilichobaki cha takribani Euro milioni 139 kikitarajiwa kutekelezwa kupitia
taasisi teule za EU, nchi wanachama, na asasi za kiraia.
Pia,
Serikali imebainisha kuwa baadhi ya hoja zilizomo katika azimio hilo hazina
uhalisia na haziakisi hatua zinazoendelea kuchukuliwa nchini baada ya matukio
ya Oktoba 2025.
Licha ya kwamba
Serikali ilitoa ufafanuzi wa kina kwa wabunge wa Bunge la Ulaya kabla ya
upigaji kura huo na kusikitishwa na hatua ya kutozingatiwa kwa maelezo hayo,
imewahakikishia wananchi kuwa uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya
Tanzania na Umoja wa Ulaya unaendelea kubaki imara na thabiti.

Post a Comment