Baraza la Vyama vya Siasa lahimiza mazungumzo yenye staha kulinda amani ya taifa
BARAZA
la Vyama vya Siasa nchini limeipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kufungua
nafasi ya majadiliano na mashauriano kati ya wadau wa kisiasa, hatua iliyotajwa
kusaidia kulinda umoja, amani na mshikamano wa taifa.
Akitoa taarifa ya maazimio ya kikao cha siku
tatu cha baraza hilo kilichomalizika Juni 18, 2026 mjini
Morogoro, Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Juma Ali Khatib
alisema wajumbe wamekubaliana kuendelea kuhimiza mazungumzo yenye staha na
kuepuka kauli zinazoweza kuleta mgawanyiko nchini.
Kikao
hicho kilihudhuriwa na wajumbe kutoka vyama 18 kati ya 19 vyenye usajili
kamili, wakiwemo wenyeviti wa vyama, makatibu wakuu, viongozi wa wanawake na
wajumbe wengine waalikwa.
Khatib alisema
baraza lina imani kuwa Tanzania itaendelea kuwa nchi moja, yenye umoja na
mshikamano.
Alisisitiza kuwa
baraza hilo linaipongeza serikali kwa kufungua milango ya mashauriano, na
akatoa wito wa kuendelea kujenga maridhiano huku wakiepuka lugha zinazoweza
kuwagawa wananchi.
Aliongeza
kuwa baraza limebaini kuwepo kwa baadhi ya kauli kutoka kwa viongozi wa kisiasa
ambazo hazijengi umoja wa taifa na kuwataka viongozi wote kuzingatia maadili ya
uongozi kwa maslahi mapana ya nchi.
Aidha, alisema
jukumu la baraza ni kuishauri serikali kwa lugha ya staha na kwamba serikali
imeendelea kuonesha usikivu kwa kupokea na kufanyia kazi ushauri unaotolewa,
hususan katika kipindi cha uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Awali, akifungua
warsha hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano),
Deus Sangu aliwataka viongozi wa vyama vya siasa kuwa mabalozi wa amani, umoja
na utulivu.
Post a Comment