WABUNGE WASIFU USIKIVU WA SERIKALI
WABUNGE
wamepongeza marekebisho yaliyofanywa na serikali katika Muswada wa Sheria ya
Fedha wa Mwaka 2026 yaliyoleta nafuu kubwa kwa wananchi baada ya serikali
kukubali mapendekezo yaliyotolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti.
Pia,
wameipongeza serikali kwa kusikiliza maoni ya bunge na wadau kwa kuondoa au
kurekebisha baadhi ya hatua za kodi zilizokuwa zimezua wasiwasi.
Miongoni
mwa mabadiliko yaliyopokelewa kwa furaha zaidi ni kuondolewa kwa ushuru wa
bidhaa wa asilimia tano uliopendekezwa kutozwa kwa pikipiki na kufutwa kwa
mpango wa kuongeza ada ya usajili wa pikipiki kutoka Sh 95,000 hadi Sh 150,000.
Akichangia,
Mbunge wa Mbarali, Bahati Ndingo (CCM) alisema serikali imeonesha usikivu kwa
kukubali mapendekezo ya kamati hiyo.
Mbunge
wa Ludewa, Joseph Kamonga (CCM) alisema bunge limefanikiwa kuishawishi serikali
kuondoa vifungu ambavyo vingewaongezea wananchi mzigo usio wa lazima.
Mbunge
wa Viti Maalumu, Dk Pindi Chana (CCM) alipongeza kuondolewa kwa ushuru
uliopendekezwa kwa sukari inayozalishwa nchini, akisema hatua hiyo ingeweza
kuchochea mfumuko wa bei na kuongeza gharama za vyakula.
“Watanzania
ni zaidi ya milioni 64 na karibu kila familia hutumia sukari kila siku.
Ongezeko lolote la kodi ya sukari lingeathiri bei za vyakula na bidhaa
zinazouzwa na wajasiriamali wadogo,” alisema.
Dk
Pindi alipongeza mageuzi yanayoruhusu asilimia tano ya mapato ya ndani ya
mamlaka za serikali za mitaa kutengwa kwa ajili ya kuboresha miundombinu
inayowawezesha wanawake wafanyabiashara na wajasiriamali.
Kwa
mujibu wake, fedha hizo zitasaidia kuboresha masoko, barabara na huduma za
usafi, hivyo kuimarisha mazingira ya biashara kwa wanawake.
Mbunge
wa Kinondoni, Abbas Tarimba (CCM) alisema ameridhishwa na utayari wa serikali
wa kusikiliza wabunge na kufanya marekebisho ya mapendekezo yaliyozua mjadala.

Post a Comment