KUMEKUCHA ZIFF ZANZIBAR: PAZIA KUFUNGULIWA KWA MAANDAMANO NA FILAMU YA SMALL GODS
Visiwa vya marashi ya karafuu viko tayari kushuhudia mchanganyiko wa kipekee wa sanaa, utamaduni na teknolojia wakati Tamasha la Kimataifa la Filamu la Zanzibar (ZIFF 2026) litakapofungua rasmi pazia lake siku ya Jumatano, Juni 24, 2026.
Tamasha hili, ambalo limebeba hadhi kubwa barani Afrika, linatarajiwa kuanza kwa kishindo kikubwa kupitia matukio mbalimbali yatakayopamba mitaa ya kihistoria ya Mji Mkongwe.
Akizungumza na BSKY Media Mtendaji wa Tamasha hilo, Jopseh Albam Mwale amesema sherehe za ufunguzi zitaanza majira ya alasiri kwa maandamano makubwa ya kitamaduni na kisanii, yakihusisha wasanii, wadau wa filamu, na wananchi mbalimbali.
Alisema maandamano hayo yataanzia eneo la Kisonge na kupita katika mitaa mbalimbali ya mji kuelekea eneo kuu la matukio (Main Event Place) katika Viwanja vya Forodhani. Maandamano hayo ya aina yake yanatarajiwa kupokelewa rasmi na Mkuu wa Wilaya ya Mjini Unguja, Mh. Saidi Haji Mrisho, hatua inayoweka muhuri wa kiserikali katika kuunga mkono tasnia ya ubunifu.
Aidha Mwale alisema Pazia la tamasha litakapofunguliwa rasmi jioni hiyo, jukwaa kuu litapambwa na uwepo wa Mgeni Rasmi, Balozi wa Italia nchini Tanzania, Mh. Giuseppe Sean Coppola.
Uwepo wake unadhihirisha uhusiano mkubwa wa kitamaduni na kidiplomasia unaoendelea kukua kupitia jukwaa la ZIFF, ambalo limekuwa likikutanisha mataifa mbalimbali duniani kubadilishana uzoefu wa sanaa ya uigizaji na utengenezaji wa filamu.
Baada ya hotuba na itifaki za ufunguzi kukamilika, macho yote yatahamia kwenye skrini kubwa ambapo watazamaji watashuhudia tukio la kihistoria la uzinduzi wa kwanza kabisa duniani (World Premiere) wa filamu ya "Small Gods" (dakika 106) kutoka nchini Uganda, iliyoongozwa na Asher Rosen.
Filamu hii yenye hisia kali inayoangazia harakati za jamii ya asili ya Wabatwa, itafungua rasmi tamasha hilo na kuwakaribisha wapenzi wa sinema katika msimu huu mpya.
ZIFF ni nini?:
Zanzibar International Film Festival (ZIFF), linalojulikana pia kama Festival of the Dhow Countries, lilianzishwa mwaka 1997 na limekuwa moja ya matamasha makubwa na yenye hadhi ya juu zaidi ya sanaa na utamaduni barani Afrika.
Lengo lake kuu ni kukuza na kuonyesha filamu na sanaa kutoka Afrika, nchi za ukanda wa Bahari ya Hindi, na diaspora ya Kiafrika, huku likiwa kichocheo kikubwa cha utalii na uchumi wa utamaduni visiwani Zanzibar.
Huu ni msimu wa 29 tangu kuanzishwa kwake, likiwa limedumu kwa karibu miongo mitatu likisika kama daraja imara la wasanii na waongozaji wa filamu duniani.
Maudhui (Theme) ya Mwaka Huu:
Katika msimu huu wa 2026, ZIFF inakwenda sambamba na mabadiliko ya kidijitali duniani ambapo maudhui makuu ni “AI and the Art of Storytelling” (Akili Unde na Sanaa ya Kusimulia Hadithi).
Maudhui haya yanajikita katika kuangazia namna teknolojia ya kisasa ya AI inavyochagiza na kubadilisha ulimwengu wa utengenezaji wa filamu na uandishi wa hadithi, bila kupoteza utambulisho na asili ya kitamaduni.

Post a Comment