TANZANIA NA NAMIBIA ZAANZA SAFARI MPYA YA USHIRIKIANO WA KIUCHUMI; ZASAINI HATI NNE ZA MAKUBALIANO IKULU DAR ES SALAAM




Na Mwandishi Wetu, BSKY Media

Tanzania na Namibia zimekubaliana kuendeleza uhusiano wao wa kihistoria uliotokana na harakati za ukombozi kwa kuupa mwelekeo mpya wa ushirikiano wa kiuchumi kupitia biashara na uwekezaji katika sekta za kimkakati. 

Makubaliano hayo yamefikiwa Juni 20, 2026, katika Ikulu ya Dar es Salaam, wakati wa ziara ya kitaifa ya Rais wa Jamhuri ya Namibia, Mheshimiwa Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah, kufuatia mwaliko wa mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Wakizungumza na waandishi wa habari, viongozi hao wamesema Tanzania na Namibia zina wajibu wa kuendeleza urithi wa ukombozi kwa kuutafsiri kuwa fursa za kiuchumi, ajira na ustawi wa wananchi wa pande zote mbili. 



Rais Dkt. Samia amebainisha kuwa nchi hizo zimekuwa zikitajataja sana uhusiano wa kihistoria, na sasa ni wakati muafaka wa kufanya uhusiano huo ulete faida za kiuchumi kwa nchi zote mbili, kwani licha ya kuwa na misingi imara ya kisiasa na kihistoria, kiwango cha sasa cha biashara na uwekezaji bado hakiendani na fursa halisi zilizopo.

Kwa upande wake, Rais Nandi-Ndaitwah ameeleza kuwa Tanzania ina nafasi ya kipekee kabisa katika historia ya Namibia kutokana na mchango wake mkubwa kwenye harakati za ukombozi pamoja na kulea viongozi wengi wa kizazi cha ukombozi wa nchi hiyo. 

Alipongeza pia ukuaji imara wa uchumi wa Tanzania na mchango wake kama mshirika muhimu wa maendeleo katika ukanda wa Kusini mwa Afrika (SADC), akitolea mfano jinsi Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia inavyoendelea kuwa mfano wa utulivu, demokrasia na ushirikiano wa kikanda.









Kwa mujibu wa Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu Bakari S. Machumu katika mazungumzo yao ya kina, viongozi hao wamekubaliana kukuza ushirikiano katika sekta mbalimbali zikiwemo biashara, uwekezaji, uchumi wa buluu, mafuta na gesi, kilimo, mifugo, uvuvi, madini, afya, elimu, utalii, usafiri wa anga, vijana, utamaduni na lugha ya Kiswahili. 

Katika sekta hizi, Tanzania imebainisha utayari wake wa kujifunza kutoka Namibia katika sekta ya uvuvi na uchumi wa buluu. Marais hao pia wamekubaliana kuharakisha utekelezaji wa makubaliano yaliyopo, ikiwemo kuanzisha safari za ndege kati ya nchi hizo mbili, pamoja na kuimarisha ushirikiano wa karibu kwenye masuala ya kikanda na kimataifa.

Kama sehemu ya uthibitisho wa kivitendo wa ushirikiano huo, viongozi wote wawili wameshuhudia utiaji saini wa hati nne za makubaliano ya ushirikiano katika masuala ya biashara, maendeleo ya biashara ndogo na za kati, ulinzi, pamoja na ushirikiano wa miji kati ya Zanzibar na Manispaa ya Swakopmund ya nchini Namibia. Hatua hii inalenga kufungua milango rasmi ya kisheria na kitaasisi ili kuruhusu sekta zote kunufaika na fursa zilizopo.

Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia na Rais Nandi-Ndaitwah wameshiriki katika Jukwaa la Biashara na Uwekezaji la Tanzania na Namibia lililofanyika katika Hoteli ya Johari Rotana, Dar es Salaam, ambalo lilikutanisha wafanyabiashara na wawekezaji wa nchi zote mbili. 

Akizungumza jukwaani hapo, Rais Dkt. Samia amesema kuwa Tanzania inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na kuikaribisha sekta binafsi ya Namibia kutumia nafasi ya Tanzania kama lango kuu la masoko ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini. Alitaja fursa zilizopo kwenye bandari, usafirishaji, kilimo na uongezaji thamani, mifugo, uvuvi, mafuta na gesi, madini, viwanda na huduma.



Naye Rais Nandi-Ndaitwah alisisitiza kuwa mafanikio ya ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Namibia hayatapimwa kwa idadi ya makubaliano yaliyosainiwa, bali yatapimwa kwa kiwango cha uwekezaji, biashara na ajira zitakazotokana na ushiriki thabiti wa sekta binafsi. 

Alitoa rai kwa sekta binafsi kutumia jukwaa hilo kugeuza fursa zilizopo kuwa viwanda na ajira, huku wakijenga daraja jipya la biashara kati ya Afrika Mashariki na Kusini. 

 "Tuhame kutoka fursa kwenda uzalishaji, kutoka majadiliano kwenda vitendo, na kujenga ushirikiano utakaoleta ajira na maendeleo kwa watu wetu." alisema.

No comments