Benki ya CRDB Yaibeba AFCON 2027, Dk Nsekela Aahidi Ushirikiano Utakaotingisha Dodoma hadi Afrika Mashariki



Benki ya CRDB imeahidi kuunga mkono maandalizi ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027) ikijiweka kama mshirika mkuu wa sekta binafsi katika jitihada za kufanikisha mashindano hayo makubwa barani Afrika. 

Ahadi hiyo ilitolewa juzi na Ofisa Mtendaji Mkuu wa benki hiyo, Dk Abdulmajid Nsekela alipotembelea banda la Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwenye maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali mkoani Dodoma.

Dk Nsekela alisema kuwa benki hiyo ipo tayari wakati wowote kushirikiana kwa karibu sana na serikali pamoja na wadau wengine ili kufanikisha maandalizi yote ya michuano hiyo ya kihistoria. Alisisitiza kuwa CRDB itakuwa bega kwa bega na wizara pale msaada wao utakapohitajika, kwani wao ni wadau wakubwa wa maendeleo ya michezo na sekta nyingine nchini na wamejitolea kikamilifu kuchangia mafanikio ya AFCON 2027.

Kiongozi huyo pia aliipongeza wizara kwa kutumia maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kama jukwaa zuri la kushirikisha wananchi na kuboresha upatikanaji wa huduma. Alibainisha kuwa ushiriki wa taasisi mbalimbali zilizo chini ya wizara hiyo umewezesha wananchi wengi kupata taarifa muhimu na huduma mbalimbali kwa ufanisi mkubwa zaidi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu wa wizara hiyo, Savera Salvatory aliikaribisha kwa mikono miwili benki hiyo na kuishukuru huku akiielezea CRDB kama mshirika nguzo na muhimu sana katika kukuza maendeleo ya michezo pamoja na sekta nyingine zote za kijamii hapa nchini.

No comments