JAB YASISITIZA UMAHIRI WA WAANDISHI KURIPOTI FURSA ZA MAENDELEO
Wakati Tanzania ikiendelea kutumia majukwaa ya kimataifa kama Maonesho ya Kiswahili nchini Ufaransa kutangaza mazao, uwekezaji na fursa mbalimbali za maendeleo, Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) imesisitiza umuhimu wa waandishi wa habari kujengewa uwezo wa kuripoti kwa umahiri masuala ya sekta maalum ili wananchi na wadau waweze kunufaika ipasavyo na taarifa hizo.
Msisitizo huo umetolewa tarehe 22 Juni, 2026 na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa JAB, Wakili Patrick Kipangula, wakati akizungumzia nafasi ya waandishi wa habari katika kuitangaza Tanzania kupitia majukwaa mbalimbali ya kimataifa, ikiwemo Kongamano na Maonesho ya Kiswahili yatakayofanyika nchini Ufaransa.
Amesema fursa zinazopatikana katika sekta za kilimo, biashara, uwekezaji, utalii na uchumi zinahitaji kuripotiwa na waandishi wenye taaluma, uelewa wa kutosha na uwezo wa kufanya uchambuzi unaozingatia maslahi mapana ya Taifa.
Amesema maonesho, makongamano na majukwaa mengine ya kimataifa yanayohusisha Tanzania yanapaswa kutazamwa kama fursa za kiuchumi na maendeleo, hivyo yanahitaji kuripotiwa kwa kina ili wananchi waelewe manufaa, changamoto na fursa zinazoweza kupatikana kupitia ushiriki wa nchi katika matukio hayo.
Kwa mujibu wa Wakili Kipangula, taarifa za kitaalamu na zenye uchambuzi zinaweza kusaidia kuvutia wawekezaji, kufungua masoko mapya ya bidhaa za Tanzania na kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu nafasi yao katika kunufaika na fursa zinazojitokeza ndani na nje ya nchi.
Amesema JAB, ambayo ni miongoni mwa taasisi zinazotarajiwa kushiriki Kongamano la Kiswahili nchini Ufaransa, itaendelea kuandaa na kuhamasisha mafunzo mbalimbali ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari ili waweze kujikita zaidi katika uripoti wa sekta maalum.
Kwa mujibu wa mwongozo wa kongamano hilo, maonesho yatatoa nafasi kwa washiriki kuonesha historia, utamaduni, lugha ya Kiswahili pamoja na fursa za maendeleo na uwekezaji zinazopatikana katika nchi zao, hatua inayotarajiwa kuvutia ushirikiano wa kimataifa katika sekta mbalimbali za uchumi.
Aidha, sehemu maalum ya maonesho itajikita katika kuonesha historia ya uhuru wa Tanzania, hatua za kuundwa kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar pamoja na mchango wa Tanzania katika harakati za ukombozi wa mataifa mbalimbali ya Afrika.
Kauli ya Wakili Kipangula inakuja wakati Tanzania ikijiandaa kushiriki Maonesho ya Kiswahili yatakayofanyika nchini Ufaransa, ambapo sekta mbalimbali za maendeleo ikiwemo kilimo zinatarajiwa kupata jukwaa la kimataifa la kutangaza fursa za biashara za mazao, uwekezaji na ushirikiano wa kiuchumi.

Post a Comment