VURUGU SABASABA HAZITAVUMILIWA


Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amesema hakuna nafasi ya watu wenye nia ya kuvuruga amani katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), akisisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaobainika kufanya vurugu.

Chalamila ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), ambapo amesema vyombo vya dola kwa kushirikiana na wananchi vimejipanga kuhakikisha ulinzi na usalama unaimarishwa kabla na wakati wa maonesho hayo.

Amesema maonesho ya Sabasaba ni tukio muhimu la kitaifa linaloonesha utajiri, utamaduni na uwezo wa kiuchumi wa Tanzania, hivyo ni wajibu wa kila mwananchi kuyalinda na kuyatumia kama fursa ya biashara, elimu na maendeleo.

Aidha, amewataka wananchi kushirikiana na vyombo vya usalama kwa kutoa taarifa za mapema kuhusu watu wenye dalili za kuvuruga amani ili hatua zichukuliwe kabla ya madhara kutokea.

Maonesho hayo yanatarajiwa kuanza Juni 28, 2026 na kufunguliwa rasmi Julai 3, 2026 katika viwanja vya Julius Nyerere (Sabasaba), Dar es Salaam.

No comments