ZAMBIA YAJA KUJIFUNZA UMEME VIJIJINI TANZANIA
Viongozi kutoka Mamlaka ya Umeme Vijijini (REA) ya Zambia wametembelea Tanzania kujifunza namna miradi ya umeme vijijini inavyotekelezwa na kufanikisha upatikanaji wa huduma hiyo katika vijiji vyote vya Tanzania Bara.
Ujumbe huo ukiongozwa na Mtendaji Mkuu wa REA Zambia, Mhandisi Alex Mbumba, umetembelea miradi ya umeme vijijini katika Kijiji cha Vikonje mkoani Dodoma kwa lengo la kujionea utekelezaji wa miradi hiyo na athari zake katika kuboresha maisha ya wananchi.Mhandisi Mbumba amesema tangu walipowasili nchini wamekuwa na vikao mbalimbali na viongozi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Tanzania ili kujifunza mbinu na uzoefu uliowezesha nchi kufikisha umeme katika vijiji vyote.
Kwa upande wake, Meneja wa Usimamizi wa Miradi ya Umeme Vijijini kutoka REA Tanzania, Mhandisi Deogratius Nagu, amesema ujio wa ugeni huo ni fursa ya kubadilishana uzoefu kuhusu utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini.
Amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi chache barani Afrika zilizofanikiwa kufikisha umeme katika vijiji vyote vya Tanzania Bara, hali iliyovutia nchi nyingine ikiwemo Zambia kufika na kujifunza namna mafanikio hayo yalivyopatikana.


Post a Comment