Upanuzi wa Vyuo vya VETA: Mkakati wa Serikali Utakavyofuta Changamoto ya Ukosefu wa Ajira
Na Mwandishi Wetu
Uwekezaji
mkubwa unaofanywa na serikali katika kupanua elimu ya ufundi stadi nchini
unatajwa kuwa mwarobaini utakaomaliza kabisa changamoto ya ukosefu wa ajira kwa
vijana na kuwazika katika shughuli za uzalishaji mali, kupitia ujenzi na
ukarabati wa miundombinu ya vyuo vya VETA.
Hatua hii
itawawezesha vijana wengi kote nchini kupata ujuzi wa vitendo utakaowaondoa
vijiweni na kuwapa fursa ya kujiajiri au kuajiriwa kwa urahisi.
Naibu Waziri wa
Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidhi Ameir, aliliambia bunge kuwa mkakati
huo unatekelezwa kupitia Mradi wa Pili wa Elimu na Ujuzi kwa Ajira Zenye Tija
(ESPJ II), unaolenga kuwabadilisha vijana kuwa nguvu kazi yenye tija na yenye
shughuli za kufanya muda wote.
Katika
kuhakikisha vijana maeneo ya vijijini wanajazwa ujuzi na kuwa 'bize' na kazi,
serikali imetenga shilingi bilioni 1.8 kwa ajili ya kukarabati Chuo cha VETA
Ulyankulu mkoani Tabora.
Akijibu swali la
Mbunge wa Ulyankulu, Japhael Lufungija, Naibu Waziri Wanu alieleza kuwa kazi za
awali zikiwemo za majengo ya utawala na karakana zimeshakamilika kwa asilimia
93.5, hatua itakayofungua milango kwa vijana wengi wa eneo hilo kupata ujuzi
utakaowaingiza moja kwa moja kwenye sekta ya uzalishaji na kuachana na
utepetevu.
Wakati
huo huo, mkakati huo unaenda sambamba na ukamilishaji wa Chuo cha VETA Wilaya
ya Kigamboni mwezi Agosti 2026, ambacho kitakuwa kimbilio la vijana wa Dar es
Salaam wanaosaka ujuzi utakaowaondoa kwenye utegemezi.
Akijibu swali la
Mbunge wa Kigamboni, Faustine Ndugulile (aliyetajwa kama Haran Sanga bungeni),
Wanu alisema serikali imetenga shilingi bilioni 2.34 kwa ajili ya vifaa vya
mafunzo nchi nzima, ambapo shilingi milioni 36 zitaenda Kigamboni ili vijana
wakute kila kitu tayari, jambo litakalowapa motisha ya kujikita kwenye masomo
ya ufundi na hatimaye kuanzisha karakana na biashara zao.
Ujenzi
huu wa Kigamboni ni sehemu ya mpango kabambe wa serikali wa kujenga vyuo 65 vya
VETA katika wilaya 64 pamoja na Mkoa wa Songwe, maeneo ambayo hapo awali
yalikuwa hayana fursa hizo.
Kusogezwa huku
kwa vyuo vya ufundi katika ngazi ya wilaya kunatarajiwa kubadilisha kabisa
mtindo wa maisha ya vijana nchini, kwani kutawapa mazingira ya kujifunza kazi
za mikono, kuwatoa kwenye wimbi la uhalifu na unyanyasaji, na badala yake
kuwapa maisha mapya yenye misingi imara ya kiuchumi kupitia ajira za uhakika.

Post a Comment