Haja ya Utulivu, Demokrasia na Amani Katika Kufanikisha Mchakato Endelevu wa Katiba Mpya Nchini
Serikali
imesisitiza kuwa mchakato wa kupata Katiba Mpya unahitaji utulivu wa kisiasa,
amani, na misingi thabiti ya kidemokrasia ili uweze kutekelezwa kwa tija,
ikibainisha kuwa jambo hilo litafanyika wakati mwafaka kulingana na taratibu
zilizowekwa.
Hatua hiyo
inalenga kuhakikisha kuwa sheria mama ya nchi inatokana na mahitaji mapana ya
Watanzania wote na si matakwa ya kundi fulani au chama kimoja cha siasa.
Waziri wa Katiba
na Sheria, Dk. Juma Homera, alieleza hayo wakati akifafanua msimamo wa serikali
kufuatia hatua ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kutangaza kamati
ya kuanza mchakato huo ndani ya siku 90, akihimiza umuhimu wa wananchi kuwa na
subira wakati serikali ikitekeleza mpango huo kwa utulivu ndani ya ratiba yake
ya miaka mitano.
Dk.
Homera alisema kuwa Tanzania ni nchi inayozingatia uhuru wa kutoa maoni na
kwamba makundi yote yana haki ya kuchangia mawazo yao kuhusu masuala ya
kitaifa, mradi tu wafanye hivyo kwa kufuata sheria ili kulinda amani iliyopo.
Alibainisha kuwa
suala la Katiba Mpya limeainishwa wazi katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM) na limekuwa likizungumzwa na Rais Samia Suluhu Hassan, ikiwa ni
pamoja na kugusiwa kwenye mapendekezo ya Tume Huru ya uchunguzi wa matukio ya
uvunjifu wa amani yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29,
2025.
Hii inaonesha
kuwa dhamira ya serikali ipo palepale, lakini inahitaji mazingira yenye utulivu
ili kufanya maamuzi sahihi ya kikatiba kwa maslahi ya taifa zima.
Wakati
serikali ikihimiza mwelekeo huo wa kisheria na utulivu, Chadema kupitia Katibu
Mkuu wake, John Mnyika, imetangaza kamati ya wajumbe 11 itakayoongozwa na
Mwenyekiti Dk. Rugemeleza Nshara na Katibu Deogratius Mainyira, ikiwa na jukumu
la kuandaa mkakati na rasimu ya muswada wa kukwamua mchakato huo kabla ya mwaka
2027.
Kamati hiyo,
inayohusisha pia wataalamu washauri wasio wanachama wa chama hicho, imepanga
kukutana na asasi za kiraia, taasisi za dini, na wadau mbalimbali ili kukusanya
maoni.

Post a Comment