Uchumi wa Taifa waimarika na kufikia ukuaji wa asilimia 5.9
Hali ya uchumi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeonesha ustahimilivu na ukuaji mkubwa katika kipindi cha mwaka 2025 ambapo pato halisi la taifa limekua kwa wastani wa asilimia 5.9 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 5.6 uliorekodiwa katika mwaka 2024.
Hatua hii ya mafanikio inatokana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu kukamilisha maboresho ya takwimu za Pato la Taifa kwa kutumia mwaka 2019 kama mwaka wa kizio badala ya mwaka 2015.
Kutokana na mabadiliko hayo, ukubwa wa pato la taifa kwa bei za mwaka 2019 umefikia shilingi trilioni 234.104 sawa na dola za Marekani bilioni 91.81 ikilinganishwa na shilingi trilioni 211.975 katika mwaka uliotangulia.
Akizungumza Bungeni leo kuhusu hali ya uchumi wa taifa kwa mwaka 2025 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa mwaka 2026 hadi 2027, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Prof Kitila Mkumbo amesema mwelekeo huo chanya umeongeza wastani wa pato la taifa kwa kila mtu kwa asilimia 7.4 ambapo sasa umefikia shilingi milioni 3.54 sawa na dola 1,390 kwa mwaka 2025 ikilinganishwa na shilingi milioni 3.29 katika mwaka 2024.
Sekta zilizochangia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji huo ni pamoja na kilimo kilichoongoza kwa kuchangia asilimia 24.3, kikifuatiwa na ujenzi kwa asilimia 11.9, uchimbaji madini na mawe kwa asilimia 10.3, biashara na matengenezo kwa asilimia 8.6, pamoja na usafirishaji na uhifadhi wa mizigo uliochangia asilimia 8.3 ya pato ghafi la taifa.
Serikali imepanga kuongeza kasi ya ukuaji huo ili kufikia asilimia 6.3 katika mwaka 2026, huku ikidhibiti mfumuko wa bei ubaki katika wigo wa asilimia 3.0 hadi 5.0 ili kulinda nguvu ya manunuzi ya wananchi.
Post a Comment