Mapinduzi makubwa katika huduma za afya, maji na elimu
Ustawi wa jamii na maisha ya wananchi wa Tanzania umeendelea kuimarika kwa vitendo kufuatia matokeo ya utafiti mpya wa mapato na matumizi ya kaya binafsi wa mwaka 2025 uliofanywa kwa pamoja pande zote za Muungano.
Takwimu zinaonesha kuwa idadi ya Watanzania wanaoishi katika umaskini wa mahitaji ya msingi kwa Tanzania Bara imepungua hadi kufikia asilimia 25.1 kutoka asilimia 26.4 ya mwaka 2018 na asilimia 28.2 ya mwaka 2012.
Sambamba na kupungua kwa umaskini, sekta ya afya imepata mafanikio ya kihistoria ambapo uwiano wa vifo vya akina mama wajawazito umeshuka kwa kasi kubwa hadi kufikia vifo 104 kwa kila vizazi hai 100,000 katika mwaka 2025 ikilinganishwa na vifo 556 vilivyorekodiwa mnamo mwaka 2021.
Akizungumza Bungeni leo kuhusu hali ya uchumi wa taifa kwa mwaka 2025 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa mwaka 2026 hadi 2027, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Prof Kitila Mkumbo amesema katika sekta ya elimu, kiwango cha ujuzi wa kusoma na kuandika kimepanda hadi asilimia 85.1 huku idadi ya wanafunzi wanaohitimu katika vyuo vikuu ikiongezeka hadi kufikia wahitimu 62,570.
Mapinduzi haya yameenda sambamba na uwekezaji mkubwa katika sekta ya maji ambapo hadi kufikia Desemba 2025 upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama umefikia asilimia 85.2 kwa maeneo ya vijijini na asilimia 92.5 kwa maeneo ya mijini nchini kote.
Wakati huo huo Profesa Kitila amesema serikali imekamilisha kwa mafanikio makubwa maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 pamoja na nyenzo zake zote za utekelezaji, hatua inayohitimisha rasmi safari ya Dira ya mwaka 2025. Aidha amesema kukamilika kwa mpango wa maendeleo wa mwaka 2025/26 kunafungua ukurasa mpya wa kuanza utekelezaji wa Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano unaoanzia mwaka 2026/27 hadi 2030/31.
Mpango huu wa kwanza wa utekelezaji wa Dira 2050 umebeba dhima kuu ya kuleta mageuzi kwa ajili ya ukuaji jumuishi wa uchumi na uzalishaji wa ajira kwa wananchi.
Katika kuelekea utekelezaji huo, serikali imeainisha maeneo makuu matano ya kipaumbele yatakayopewa msongo wa kipekee ikiwemo kuimarisha utawala bora, demokrasia, amani na utulivu, pamoja na kujenga uchumi imara, jumuishi na shindani.
Lengo kuu la dira hii mpya ni kuhakikisha kuwa kasi ya ukuaji wa uchumi inaenda sambamba na uumbaji wa fursa nyingi za ajira, ambapo kwa kuanzia katika mwaka 2026 serikali imeweka shabaha ya kuongeza uzalishaji wa ajira rasmi nchini zifikie 1,700,000 kutoka ajira 981,000 pekee zilizozalishwa katika mwaka 2024.
Post a Comment