Kitila Ataja Fursa Nne kwa Tanzania Katikati ya Mgogoro wa Mashariki ya Kati




Serikali imebainisha kuwa pamoja na mtikisiko wa kiuchumi unaoendelea duniani kutokana na vita, Tanzania ina nafasi ya dhahabu ya kugeuza migogoro hiyo kuwa fursa kubwa za kiuchumi na uwekezaji. 

Hayo yamebainishwa bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, wakati akiwasilisha Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2025 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027.

Profesa Kitila alisema kuwa dunia kwa sasa inashuhudia misukosuko mizito ya kisiasa na kiuchumi inayotokana na vita vya Urusi na Ukraine, pamoja na vile vinavyoihusisha Marekani na Israel dhidi ya Iran. Hali hii imeathiri kwa kiasi kikubwa sekta za biashara, uwekezaji, na minyororo ya usambazaji wa bidhaa duniani kote.

Hata hivyo, Profesa Kitila alifafanua kuwa Tume ya Taifa ya Mipango kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa walifanya utafiti maalum ulioonesha fursa mbalimbali ambazo Tanzania inaweza kuzichangamkia. 

Fursa ya kwanza ni kuongeza uzalishaji wa ndani wa bidhaa ambazo upatikanaji wake katika masoko ya kimataifa umepungua au kuathiriwa na vita hivyo vya Mashariki ya Kati.

Fursa nyingine kubwa ipo katika kuboresha huduma za bandari na uhifadhi, ambapo Tanzania inaweza kutoza na kutoa huduma ya kupakua na kuhifadhi mizigo kwa muda kwa ajili ya meli kubwa zilizoshindwa kutia nanga au kufikisha shehena zake katika bandari za Mashariki ya Kati kutokana na usalama mbovu. 

Aidha, nchi ina nafasi ya kipekee ya kuwavuta wawekezaji wa kimataifa wanaotafuta maeneo salama na yenye utulivu wa kisiasa ili kuwekeza mitaji yao, hususan katika sekta ya gesi asilia.

Akiitaja mifano ya athari za mgogoro huo, Waziri Kitila alisema vita dhidi ya Iran vilivyoanza Februari 2026 vilileta taharuki kubwa katika soko la nishati kwa hofu ya kuvurugika kwa njia za usafirishaji katika Ghuba ya Uajemi. 

Hali hiyo ilisababisha bei ya mafuta ghafi kupanda kutoka dola za Marekani 100 kwa pipa mwezi Machi hadi kufikia dola 126 mwezi Aprili 2026, kabla ya kuanza kushuka na kutulia kati ya dola 90 na 95 kwa pipa mwanzoni mwa Juni mwaka huu. Aliongeza kuwa kubadilishwa kwa njia za meli ili kuepuka maeneo ya vita kumesababisha kupanda kwa gharama za usafirishaji na kuongeza muda wa bidhaa kufika sokoni.

Kwa upande wa Tanzania, athari kubwa zimeonekana kwenye sekta za kilimo, viwanda, biashara, nishati na uchukuzi kutokana na utegemezi wa masoko hayo. 

Kwa mfano, taifa huagiza kati ya asilimia 30 hadi 40 ya mbolea aina ya Urea na DAP kutoka nchi za Ghuba, hasa Qatar, na usumbufu wa vita unaweza kupandisha bei ya mbolea hiyo katika msimu wa kilimo wa 2026/2027. Vilevile, nchi inategemea uagizaji wa mafuta yaliyosafishwa kwa asilimia 100 kutoka nje, ambapo kati ya asilimia 60 hadi 70 ya nishati hiyo hutoka nchi za Ghuba, India, na Singapore.

Ili kulinda uthabiti wa uchumi wa nchi dhidi ya dhoruba hizo za nje, Profesa Kitila alieleza kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti za kijihami. 

Hatua hizo ni pamoja na kuimarisha na kuoanisha sera za fedha na bajeti, kuhamasisha kwa kasi matumizi ya nishati mbadala kama gesi asilia na umeme, kuongeza kiwango cha akiba ya kimkakati ya mafuta nchini, pamoja na kuwapa motisha wazalishaji wa ndani ili kuongeza uzalishaji wa bidhaa muhimu na kupunguza utegemezi wa masoko ya nje

No comments