Sheria mpya FIFA ‘yamlamba’ nahodha Paraguay
SAN FRANCISCO, Marekani.
Nahodha wa timu ya taifa ya Paraguay, Miguel Almiron ameandika historia isiyotarajiwa katika ulimwengu wa soka baada ya kuwa mchezaji wa kwanza kutolewa uwanjani kwa kadi nyekundu kutokana na kuziba mdomo wake alipokuwa akizungumza na mchezaji mpinzani. Tukio hilo la kipekee lilijiri katika mchezo wa Kombe la Dunia dhidi ya Uturuki uliochezwa mjini San Francisco nchini Marekani, ambapo nyota huyo mwenye umri wa miaka 32 alionekana akifunika mdomo wake kwa mkono alipokuwa akizungumza na beki wa Uturuki, Mert Muldur, hatua iliyomfanya mpinzani wake huyo kutoa taarifa mara moja kwa mwamuzi aliyekuwa karibu na eneo la tukio.
Baada ya kufanya marejeo ya Teknolojia ya Usaidizi wa Mwamuzi yaani VAR, mwamuzi Ivan Barton kutoka El Salvador alitangaza kuwa Almiron ametenda kosa kubwa chini ya sheria mpya ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani FIFA inayokataza wachezaji kufunika midomo yao wanapozungumza uwanjani ili kuongeza uwazi na kupiga vita vitendo vya utovu wa nidhamu na ubaguzi. Licha ya Paraguay kubaki na wachezaji kumi uwanjani kwa zaidi ya nusu ya mchezo huo tangu kabla ya mapumziko ya kipindi cha kwanza, walipambana kiume na kufanikiwa kulinda bao lao la uongozi na kukamilisha mchezo huo kwa ushindi muhimu wa bao moja kwa sifuri.
Sheria hii mpya iliyomponza Almiron ilipitishwa rasmi na Bodi ya Kimataifa ya Vyama vya Soka IFAB mwezi Aprili mwaka huu na imeanza kutumika kwa mara ya kwanza duniani katika michuano hii inayoendelea ya Kombe la Dunia la mwaka 2026. Kutokana na kadi hiyo nyekundu ya moja kwa moja, nahodha huyo sasa atalazimika kukaa nje katika mechi inayofuata na ya mwisho ya hatua ya makundi dhidi ya Australia, mchezo ambao Paraguay inahitaji kupata ushindi ili iweze kujihakikishia nafasi ya kutinga katika hatua ya 32 bora ya michuano hiyo mikubwa kabisa duniani.

Post a Comment