AFCON 2027: Simon Msuva Afunguka Mazito JAB, Aeleza Waandishi Watakavyoibeba Tanzania
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa timu ya taifa ‘Taifa Stars’, Simon Msuva amepongeza mpango wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) wa kuandaa mafunzo maalumu kwa wanahabari kuelekea mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027). Alisema hatua hiyo itasaidia kuimarisha mchango wa sekta ya habari katika kuitangaza Tanzania, kukuza vipaji vya wanamichezo na kuibua fursa mbalimbali za maendeleo zitakazotokana na mashindano hayo.
Msuva alitoa pongezi hizo juzi alipotembelea ofisi za JAB zilizopo Posta Mpya, Dar es Salaam na kufanya mazungumzo na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa bodi hiyo, Patrick Kipangula. Katika mazungumzo hayo, nyota huyo alisisitiza kuwa waandishi wa habari wamekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya michezo nchini kwa kutangaza vipaji, kuhamasisha ushiriki wa wananchi na kuitangaza nchi ndani na nje ya mipaka.
Msuva alifunguka kuwa tasnia ya habari ndiyo iliyomfikisha hapo alipo leo, kwani bila kalamu za waandishi huenda jina lake lisingekuwa kubwa kiwango hicho. Aliongeza kuwa kutokana na nafasi yao kubwa kwa taifa, kuna umuhimu mkubwa kwa wao kuendelea kupata elimu na mafunzo yatakayowasaidia kuwa bora zaidi katika kazi zao kila uchao.
Kuhusu mashindano yajayo, mshambuliaji huyo mahiri alibainisha kuwa AFCON 2027 ni zaidi ya mashindano ya mpira wa miguu. Alieleza kuwa yatatoa fursa adhimu katika sekta mbalimbali ikiwemo biashara, utalii, uwekezaji na ajira, jambo linalofanya maandalizi ya mapema kwa waandishi kuwa ya lazima ili waripoti kwa weledi na kusaidia wananchi kuzichamvua na kuzichangamkia fursa hizo.
Kwa upande wake, Patrick Kipangula alimshukuru Msuva kwa kutembelea bodi hiyo na kuunga mkono juhudi za kuimarisha taaluma ya habari nchini. Alifafanua kuwa JAB tayari imeanza maandalizi ya mafunzo hayo maalumu kwa waandishi wa michezo na kada nyingine ili kuwajengea uwezo wa kuripoti mashindano hayo kwa viwango vya kimataifa, huku wakimulika fursa za kiuchumi zitakazojitokeza.
Kipangula alihitimisha kwa kusema kuwa kupitia mafunzo hayo, waandishi watawezeshwa kuelewa kwa kina mchango wa michezo katika maendeleo ya taifa, uchumi wa michezo, utalii na uwekezaji. Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa kihistoria wa AFCON 2027 kwa kushirikiana na mataifa jirani ya Kenya na Uganda, hatua inayotazamiwa kufungua milango mikubwa ya kiuchumi na kijamii kwa ukanda mzima wa Afrika Mashariki.

Post a Comment