Dk Kasiga Ang'ara Urusi, Atangaza Washindi Eurasia-Kinofest 2026 na Kulibebea Jina la Tanzania




Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Dk Gervas Kasiga ameendelea kuitangaza sekta ya sanaa ya nchi yetu kimataifa baada ya kushiriki kikamilifu katika Tamasha la Kimataifa la Filamu la Eurasia-Kinofest la mwaka 2026 lililofanyika nchini Urusi. Tamasha hilo kubwa ambalo limekamilika hivi karibuni jijini Sochi, lilihusisha ushindani mkali wa filamu 100 kutoka katika mataifa 53 duniani kote, huku Tanzania ikipata heshima ya kipekee kupitia uwakilishi wa kiongozi huyo wa tasnia ya filamu nchini.

Katika hafla ya kufunga tamasha hilo, Dk Kasiga alipata heshima kubwa ya kuwasilisha kwa njia ya video Tuzo ya Muswada Bora wa Filamu, ambapo filamu iitwayo ‘VATA’ kutoka nchini Uzbekistan iliibuka mshindi wa kipengele hicho. Taarifa kutoka Bodi ya Filamu ilieleza kuwa fursa hiyo adhimu ilitoa nafasi ya kipekee kwa lugha adhimu ya Kiswahili, jina la Tanzania na kivutio kikuu cha Mlima Kilimanjaro kusikika na kuonekana mbele ya mamia ya wadau, waongozaji, na wawekezaji wa filamu kutoka pembe zote za dunia.

Mbali na kutoa tuzo hiyo, Dk Kasiga aliweka rekodi nyingine baada ya kuchaguliwa kuwa miongoni mwa wajumbe wa jopo la majaji katika kipengele cha filamu ndefu, akiwa ndiye Mwafrika pekee aliyeshiriki katika mchakato huo wa kitaalamu wa kutathmini na kuchagua washindi. Ushiriki huu wa kihistoria katika tamasha la Eurasia-Kinofest 2026 unaendelea kufungua milango mikubwa ya ushirikiano wa kimataifa katika sekta ya filamu, huku ukitangaza kwa nguvu uwezo, ubunifu, na nafasi ya Tanzania katika maendeleo ya tasnia ya filamu na michezo ya kuigiza duniani.

No comments