PROFESA KITILA AELEZA KUSHUKA KWA UKOSEFU WA AJIRA
.Rasilimali watu na miradi ya kielelezo inavyosukuma kasi mpya ya uchumi wa taifa
Ripoti ya Hali ya Uchumi wa Taifa imeonesha mafanikio makubwa katika soko la ajira ambapo kiwango cha ukosefu wa ajira nchini kimepungua kwa kiasi kikubwa hadi kufikia asilimia 6.2 katika mwaka 2024, ikilinganishwa na asilimia 8.7 iliyorekodiwa mnamo mwaka 2020/21.
Sambamba na hayo, wastani wa ukuaji wa ajira kwa mwaka umeongezeka kwa kasi na kufikia asilimia 7.8 mwaka 2024 ikilinganishwa na asilimia 2.3 hapo awali, huku serikali ikiweka shabaha ya kuongeza uzalishaji wa ajira kufikia 1,700,000 katika mwaka 2026 kutoka ajira 981,000 zilizozalishwa mwaka 2024.
Nguvu kazi ya taifa kwa sasa imefikia watu milioni 27.3, huku kundi kubwa la watu milioni 25.6 likiwa katika sekta yenye ujira. Katika kundi hili la wenye ujira, sekta ya kilimo bado inaongoza kwa kuajiri asilimia 54.2 ya nguvu kazi yote, ikifuatiwa na sekta ya huduma kwa asilimia 35.5, na sekta ya uzalishaji viwandani inayochukua asilimia 10.3.
Takwimu hizo zimetolewa leo Bungeni na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Prof Kitila Mkumbo wakati akiwasilisha hali ya uchumi wa taifa kwa mwaka 2025 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa mwaka 2026 hadi 2027.
Aidha alisema katika utumishi wa umma, serikali imefungulia ajira na vyeo vilivyokuwa vimesitishwa kati ya mwaka 2016 na 2020, ambapo katika miaka mitano iliyopita imeshaajiri watumishi wapya 32,833, wakiwemo walimu 7,000 na watumishi wa afya 5,000 walioajiriwa hivi karibuni.
Katika kuendeleza na kuimarisha rasilimali watu, serikali imeshuhudia mapinduzi makubwa ya kijamii ambapo ujuzi wa kusoma na kuandika miongoni mwa wananchi umepanda hadi kufikia asilimia 85.1, huku idadi ya wanafunzi wanaohitimu katika vyuo vikuu ikiongezeka hadi kufikia wahitimu 62,570 katika mwaka 2024.
Maendeleo haya ya rasilimali watu yanaenda sambamba na uboreshaji wa afya ya jamii, ambapo uwiano wa vifo vya akina mama wajawazito umepungua kwa kiwango kikubwa hadi kufikia vifo 104 kwa kila vizazi hai 100,000 katika mwaka 2025, kutoka vifo 556 vya mwaka 2021.
Ili kuwajengea vijana uwezo wa kujiajiri, Ilani ya CCM imeelekeza kukuza stadi za maisha na ujuzi kwa kujenga vyuo vya mafunzo ya amali katika kila wilaya nchini.
Mageuzi haya ya ajira na rasilimali watu yanasukumwa kwa nguvu na sekta ya kilimo pamoja na miradi mikubwa ya maendeleo ya kielelezo na kimkakati.
Sekta ya kilimo imeendelea kuwa nguzo mama baada ya kuchangia asilimia 24.3 ya Pato Ghafi la Taifa kwa mwaka 2025. Ili kuongeza tija vijijini, serikali inatekeleza mikakati 12 ikiwemo kupitia upya mifumo ya uuzaji mazao, kuimarisha usalama wa chakula, kuweka mifumo ya mikopo yenye riba ndogo, na kupanga matumizi bora ya ardhi kwa kuhakikisha angalau asilimia 60 ya ardhi ya vijiji imepimwa ifikapo mwaka 2030.
Aidha, serikali imehitimisha kwa mafanikio miradi mikubwa ya miundombinu ikiwemo reli ya kisasa ya SGR (kilomita 680.38) ambapo huduma zimeanza kati ya Dar es Salaam na Dodoma, mradi wa kufua umeme wa Julius Nyerere uliomfanya uwezo wa taifa kufikia Megawati 4,522.54, na kukamilika kwa Daraja la JPM la Kigongo–Busisi.
Aidha taifa limefungua ukurasa mpya wa Dira ya 2050 ambapo gharama za utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2026/27 unakadiriwa kuwa shilingi trilioni 86.3, ambapo sekta binafsi inatarajiwa kubeba mzigo mkubwa wa asilimia 69.6 (shilingi trilioni 60.1) kupitia programu saba za kielelezo ikiwemo mradi wa Kitaifa wa Umwagiliaji na viwanda vya uchakataji mazao, mradi wa chuma cha Liganga na makaa ya mawe Mchuchuma, kiwanda cha kuchakata gesi asilia ya kimiminika (LNG) Lindi, na kitovu cha uchakataji madini adimu Dodoma.
Post a Comment