Ukuaji wa Idadi ya Wanyamapori Nchini: Fursa ya Dhahabu ya Ajira Kwenye Mnyororo wa Thamani wa Utalii Tanzania
Na Mwandishi Wetu
Kuongezeka
kwa idadi ya wanyamapori nchini kumeendelea kufungua milango mikubwa ya ajira
na fursa za kiuchumi kwa Watanzania, huku nchi ikithibitisha nafasi yake kama
moja ya mataifa yenye utajiri mkubwa zaidi wa wanyamapori barani Afrika.
Matokeo ya Sensa
ya Kitaifa ya Wanyamapori ya Mwaka 2024/2025 yaliyozinduliwa hivi karibuni
jijini Arusha yanaonesha uwepo wa spishi 28 za wanyamapori wakubwa katika
mifumo mbalimbali ya ikolojia.
Ongezeko hili la
wanyama linamaanisha kukua kwa uhakika kwa soko la ajira katika mnyororo mzima
wa sekta ya utalii, kuanzia waongoza watalii, madereva, wafanyakazi wa hoteli
na kambi za kitalii, hadi kwa watoa huduma za usafiri na chakula.
Akizungumza
wakati wa uzinduzi wa matokeo hayo kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan,
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Ashatu Kijaji alieleza kuwa Tanzania sasa
inashika nafasi ya tatu Afrika kwa idadi ya tembo ikiwa nao 66,737, na nafasi
ya nne kwa faru weusi na weupe wanaofikia 322.
Utajiri huu wa
kipekee wa bayoanuwai, unaojumuisha pia uongozi wa Tanzania barani Afrika kwa
kuwa na nyati zaidi ya 321,437 na simba zaidi ya 17,200, unazidi kuimarisha nafasi
ya nchi kama kitovu kikuu cha utalii duniani.
Ujio mkubwa wa
watalii unaochochewa na takwimu hizi una matokeo ya moja kwa moja katika
kuongeza nafasi za kazi na vipato kwa jamii zinazozunguka hifadhi na Watanzania
kwa ujumla.
Hata
hivyo, ili kulinda mnyororo huu unaozalisha maelfu ya ajira, serikali imeonya
kuwa shinikizo la shughuli za kibinadamu katika maeneo ya ikolojia linaweza
kuhatarisha mustakabali wa sekta hiyo.
Dk. Kijaji
alibainisha kuwepo kwa migogoro kati ya binadamu na wanyamapori, akitolea mfano
Pori la Akiba la Longido ambako wanyama kama swala na twiga wameanza kupotea.
Kutokana na hali
hiyo, aliziagiza taasisi za utafiti kama Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori
Tanzania (TAWIRI) kufanya tafiti za kina kuhusu matumizi ya ardhi na athari za
kibinadamu katika korido za wanyama ili kulinda rasilimali hizi zinazolisha
uchumi wa nchi.
Mkurugenzi
Mkuu wa TAWIRI, Dk. Eblate Mjingo aliongeza kuwa juhudi za kupambana na
ujangili zimesaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza idadi ya wanyama, hususan tembo
ambao wameongezeka kutoka viwango vya chini vya miaka ya nyuma. Licha ya
mafanikio hayo, Dk. Mjingo alitahadharisha kuwa mwingiliano wa makazi ya watu,
kilimo, na ufugaji karibu na maeneo ya hifadhi kama vile Maswa na
Selous-Nyerere unavuruga njia za asili za uhamaji wa wanyama.
Changamoto hii
inatishia uendelevu wa utalii, jambo linalofanya takwimu hizi kuwa mwongozo
muhimu wa jinsi ya kubalansi uhifadhi na maendeleo ya kijamii.
Kwa
upande wao, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Hassan Abbasi, na
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Timotheo
Mzava, walisisitiza kuwa sensa hii ni zana ya kimkakati itakayosaidia kuunda
sera bora za matumizi endelevu ya ardhi na kutatua migogoro iliyopo.
Sensa hiyo ya
Mwaka 2024/2025, ambayo imefadhiliwa kwa asilimia 100 na serikali ya Tanzania,
inaweka msingi imara wa jinsi nchi inavyoweza kulinda ikolojia yake huku
ikihakikisha kuwa sekta ya utalii inaendelea kuwa mhimili mkuu wa uzalishaji wa
ajira na kukuza uchumi wa taifa.

Post a Comment