DK CHEGENI: TAIFA LINAHITAJI KUJIJENGA KATIKA AMANI, UTULIVU

 


“KAMA Mtanzania, mzalendo na mwanasiasa, taifa kwa sasa linahitaji kujijenga katika misingi imara ya mustakabali wake, ikiwemo amani, utulivu, uongozi bora na kuenzi mila na desturi.” Anasema mwanasiasa mkongwe na mbunge wa zamani wa Jimbo la Busega, Dk Raphael Chegeni katika mazungumzo ya hivi karibuni  yaliyofanyika Mwanza kuhusu mwelekeo wa Tanzania na hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kuendeleza amani, umoja na mshikamano wa kitaifa.

Anasema mambo hayo yana uhusiano wa karibu na yanaposimamiwa kwa umakini hujenga taifa lenye mwelekeo thabiti wa amani, hali inayochochea kuwapo kwa maendeleo endelevu. Anasema katika kipindi hiki ambacho mataifa mengi yanakabiliwa na misukosuko ya kisiasa, kiuchumi na kijamii, Tanzania inazidi kudumisha taswira yake ya kuwa nchi inayolinda na kuenzi tunu za amani na utulivu.

Hata hivyo, anasema mafanikio hayo hayapaswi kuchukuliwa kama jambo la kudumu bila kuwepo kwa juhudi za makusudi za kuyaendeleza. Kwa mujibu wa Dk Chegeni, kuna umuhimu wa kuimarisha maadili ya jamii, kulinda utamaduni na kuhakikisha utawala wa sheria unazingatiwa katika ngazi zote.

Anasema amani si tu kutokuwepo kwa vita, bali pia uwepo wa haki, usawa, heshima na fursa kwa wananchi wote kushiriki katika maendeleo ya nchi yao kwa ustawi wa maisha yao. Anasema mazingira yenye usawa na haki huondoa hisia za kutengwa na hivyo kupunguza uwezekano wa migogoro ya kijamii.

Akizungumzia utawala wa sheria, Dk Chegeni anasisitiza kuwa msingi wa amani ya kudumu ni uwepo wa taasisi imara zinazofanya kazi kwa uwazi na bila upendeleo. Anasema taasisi za mahakama, bunge na vyombo vya usimamizi wa haki vina jukumu la kuhakikisha sheria zinatekelezwa kwa haki kwa wananchi wote.

“Sheria zisimamiwe kwa usawa bila kujali nafasi ya mtu katika jamii,” anasisitiza. Katika eneo la uongozi, alisema viongozi wanapaswa kuwa mfano wa uadilifu, uwajibikaji na kujali maslahi ya umma. Chegeni anasema uwajibikaji unapaswa kuonekana kwa vitendo kupitia mifumo madhubuti ya kupima utendaji na kuchukua hatua dhidi ya wanaokiuka maadili ya uongozi. 

Anabainisha kuwa jamii inayokosa viongozi waadilifu mara nyingi hukumbwa na migogoro na kushuka kwa imani ya wananchi kwa taasisi za umma. Kuhusu ushirikishwaji wa wananchi, Dk Chegeni anasema ni muhimu kuhusisha uamuzi unaowahusu ili kujenga dhana ya umiliki wa pamoja wa maendeleo. 

Anasema majukwaa ya vijana, wanawake na sekta binafsi yakiboreshwa huwa njia muhimu ya kukuza ushiriki wao katika mambo muhimu ya nchi.

Kwamba, ushirikishwaji huo pia husaidia kupunguza migogoro na kuongeza uwazi, hasa katika enzi ya mitandao ya kijamii ambapo taarifa husambaa kwa kasi kubwa.

No comments