Uzoefu wa Miaka 37 ya Beda Msimbe: Watanzania Diplomasia ya Nyumbani Ndio Suluhu



Mwandishi mwandamizi na mkongwe katika tasnia ya habari nchini, Beda Msimbe, ametoa mtazamo wake wa kina kuhusu mjadala unaoendelea mtandaoni kuhusiana na ripoti ya Jaji Chande, akisisitiza umuhimu wa watanzania kutatua changamoto zao ndani ya nchi badala ya kukimbilia msaada wa nje. 

Akizungumza hivi karibuni katika kipindi cha Hotzone kinachorushwa na Kasaco Media, Msimbe amebainisha kuwa tangu alipoanza kazi ya uandishi wa habari mwaka 1985 hadi alipostaafu rasmi kwenye ajira za vyombo vya habari mwaka 2022, ameshuhudia matukio mengi ambapo nchi ilifanikiwa kuvuka vikwazo vikubwa kwa kutumia busara na mazungumzo ya ndani. 

Anahoji mantiki ya kuamini kuwa watanzania wameshindwa kuelewana kiasi cha kuhitaji waamuzi kutoka nje, akisisitiza kuwa utamaduni wa kumaliza tofauti "nyumbani" ndio umekuwa nguzo ya amani ya Tanzania kwa miongo mingi.

Katika kufafanua hoja yake, Msimbe ametumia mfano wa taasisi ya ndoa akieleza kuwa hata mume na mke wanapopata msuguano ndani ya nyumba, hatua ya kwanza si kukimbilia kwa balozi au mahakamani, bali ni kujaribu kukaa chini na kusikilizana kwanza. 

Anasema kuwa ni lazima kufikia hatua ya kukubaliana au kutokubaliana, lakini ndani ya misingi ya kifamilia kwa sababu wote ni wamoja na wanaunganishwa na majukumu ya malezi na mustakabali wa watoto wao. 

Kwa mujibu wa mwanahabari huyo, inapofika hatua wanandoa wanashindwana kabisa, taratibu za kisheria hazianzi mahakamani kudai talaka moja kwa moja, bali hupitia katika mabaraza ya usuluhishi ambayo yapo kuanzia ngazi ya kata, msikitini, au kanisani ili kutafuta suluhu ya amani kabla ya kuchukua hatua kubwa zaidi.

Msimbe amehitimisha kwa kuhoji ikiwa kweli Tanzania kama taifa imefikia hatua ya kushindwa kabisa kuelewana kiasi cha kuhitaji msaada wa watu wengine kuja kutatua matatizo ya ndani.

Amesema kuwa mfumo wa usuluhishi uliopo kuanzia ngazi ya balozi hadi mabaraza ya kata unapaswa kuheshimiwa na kutumika kama daraja la kufikia muafaka wa kitaifa. Kwa mtazamo wake, kelele za mitandaoni zinazopuuza ripoti ya Jaji Chande zinapaswa kupimwa kwa kulinganisha na uwezo wa watanzania kukaa pamoja kama familia moja na kutatua changamoto zao bila kulazimika kufika katika "mahakama" za kimataifa, jambo ambalo anaamini bado linawezekana kabisa kutokana na historia na hekima ya nchi hii.

No comments