Hatujashindwana: Watanzania Watakiwa Kupuuza 'Matapeli wa Amani' Mtandaoni
Ni vyema Watanzania wakapata ufahamu wa kina juu ya mbinu chafu zinazotumiwa na baadhi ya watu kwenye mitandao ya kijamii ambao wamejipa kazi ya kuchafua hali ya hewa ya nchi kwa manufaa yao binafsi.
Watu hawa, ambao mara nyingi hujivika joho la uzalendo bandia na wanaharakati uchwara, hutumia majukwaa kama Instagramu, WhatsApp, X, na Facebook kusambaza habari za upotoshaji na video za kizamani ili kuleta taharuki na hofu isiyo na msingi.
Wananchi wanapaswa kuelewa kuwa nchi yetu haipangwi mtandaoni na wala mwelekeo wa taifa letu hauwezi kuamuliwa na watu wanaoshinda nyuma ya vitufe vya simu wakiwahubiria chuki za kidini, kikabila, au kishabiki huku wao wakiwa wamejificha kwenye usalama wa nyumba zao.
Mtanzania mzalendo hapaswi kukubali kuyumbishwa na tetesi za mitaani wala kufuata mihemko ya kisiasa inayolenga kutugawa na kutugonganisha kwa ajili ya ajenda za siri za wachache.
Ni muhimu kupuuza jumbe zinazochochea uvunjifu wa sheria na kukataa kujiunga na mikusanyiko isiyo rasmi inayopanga fujo, kwani mara nyingi waandaaji wa vurugu hizo hubaki salama huku wananchi wa kawaida wakibaki wakiumia na kupoteza amani yao.
Badala ya kuamini kila kinachoandikwa na watu wasio na utambulisho rasmi, jamii inahimizwa kuchakata taarifa kwa makini ili kulinda utulivu wa taifa letu.
Umoja na mshikamano wetu ndio ngao pekee dhidi ya matapeli hawa wa amani wanaotumia tofauti za mawazo au ushabiki wa vyama kama silaha ya kutugawa.
Ni lazima tuwe macho na watu wageni au wenye mienendo inayotilia shaka wanaoingia mitaani mwetu kuhubiri uhasama, na badala yake tutoe taarifa kwa mamlaka husika ili kuzuia mbegu ya chuki isiote.
Tanzania ni yetu sote na maendeleo tunayoyaona chini ya uongozi wenye maono ni matokeo ya amani tuliyoichagua, hivyo tusiwakabidhi watu wa mtandaoni funguo za utulivu wetu kwani amani ya kweli inalindwa na Watanzania wenyewe wenye uchungu na nchi yao na siyo wapiga kelele wa kidijitali.

Post a Comment