Rais Samia amwomba Drogba kuwa Balozi wa Tanzania AFCON 2027
RAIS
Samia Suluhu Hassan amemuomba mshambuliaji wa zamani wa timu ya taifa ya mpira
wa miguu ya Ivory Coast na Chelsea ya England, Didier Drogba kuwa Balozi wa
Tanzania kuelekea fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027).
Kwa mujibu
wa Ikulu, ombi hilo limetolewa leo wakati nyota huyo alipowasili Ikulu ya
Chamwino mkoani Dodoma kuonana na Rais Samia.
Aidha, Rais
Samia ameitaka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kushirikiana na
Drogba kubadilishana uzoefu wa kuendesha vituo vya michezo nchini.
Drogba
aliyekuwa nchini kwa mwaliko wa waziri mwenye dhamana ya habari na michezo,
Paul Makonda amemshukuru Rais Samia na kuonesha utayari wa kushirikiana na
serikali.
Tanzania
inaandaa Afcon 2027 kwa pamoja na Kenya na Uganda na droo ya kufuzu itafanyika
Mei 19, mwaka huu. Fainali hizo zitaanza Juni 19 hadi Julai 17, 2027.
Huo ni
mwanzo wa mchakato utakaohusisha mataifa 48 yatakayopangwa katika makundi 12,
ambapo washindi wawili wa kwanza kila kundi watakata tiketi ya kucheza fainali
hizo.
Pamoja na
mafanikio kadhaa aliyoyapata katika mpira wa miguu, mwaka 2005 Drogba alifanya
ushawishi uliosaidia kusitishwa kwa vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini kwao
vilivyodumu kwa miaka kadhaa.
Drogba
baada ya kuiongoza Ivory Coast kufuzu kwa Kombe la Dunia mwaka 2006 kwa mara ya
kwanza Oktoba 8, 2005 alichukua kipaza sauti kwenye chumba cha kubadili nguo
akizungukwa na wachezaji wenzake kutoka Kaskazini na Kusini mwa nchi, akapiga
magoti mbele ya kamera ya televisheni ya taifa na kuwaomba wapiganaji waweke
silaha chini.
Ndani ya
wiki moja baada ya ombi lake, pande zote mbili zilizoingia kwenye mgogoro
zilikubali kusitisha mapigano, tukio ambalo lilionesha nguvu ya michezo katika
kuunganisha taifa.
Ili
kuimarisha zaidi amani hiyo, Drogba alishauri mechi ya kufuzu dhidi ya
Madagascar ya mwaka 2007 ichezwe katika Mji wa Bouaké, uliokuwa ngome ya waasi
na hiyo ilikuwa ishara kubwa ya maridhiano ambapo viongozi wa serikali na waasi
walikaa pamoja kushuhudia ushindi wa timu ya taifa.
.jpeg)

Post a Comment