USIKU MMOJA WA TAMASHA SHAKIRA AIZALISHIA COPACABANA BILIONI 405.9



Haikuwa tu tamasha, bali ulikuwa ni mkusanyiko wa kihistoria ulioshuhudia ladha pekee ya muziki wakati malkia kutoka Colombia, Shakira, alipoiteka fukwe ya Copacabana nchini Brazil akiwavuta  watu zaidi ya milioni mbili katika eneo la wazi lenye mchanga mweroro kushuhudia mikito ya mwanadada huyo.

Kulikuwa na mbwembwe nyingi angani pamoja na droni zilizochora maneno ya upendo akithibitisha yeye ni nembo ya dunia linapokuja suala la utumbuizaji .

Rekodi yake ililinganishwa na mastaa kama Madonna na Lady Gaga waliotumbuiza katika eneo hilo. 

Meya wa Rio de Janeiro, Eduardo Cavaliere, hakuchelewa kuandika kupitia mtandao wa X kuwa mwanadada huyo ameweka historia mpya jijini humo kupitia ziara yake ya 'Las Mujeres Ya No Lloran', jina linalobeba ujumbe mzito kutoka kwenye albamu yake ya mwaka 2024 kuwa wanawake hawalii tena (Women no Longer Cry) bali wanageuza maumivu kuwa mafanikio.

Fukwe ilinoga kwa mchanganyiko wa muziki wa mahadhi ya zamani na sasa, ambapo Shakira alicharaza vibao vyake vikali kama ‘Hips Don't Lie’ na ‘La Bicicleta’, huku akihitimisha usiku huo kwa wimbo wake maarufu wa Bizarrap ambao ni dongo kwa aliyekuwa mpenzi wake, Gerard Piqué. 

Pamoja na hayto waliwapa mashabiki wake ziada kwa kupanda jukwaani na mastaa wa Brazil kama Anitta, Caetano Veloso, na Maria Bethânia, huku akichukua muda mfupi kwa hisia kukumbuka fundi aliyepoteza maisha wakati wa maandalizi ya tamasha hilo. 

Uhusiano wake na Brazil ulionekana kuwa wa damu zaidi kuliko biashara, kwani mwimbaji huyo alikumbushia safari yake ya kwanza nchini humo akiwa na miaka 18 tu na ndoto kubwa, jambo ambalo wataalamu wa muziki wanalielezea kama kilele cha ukaribu wa kitamaduni kati ya nchi hizo mbili.

Wakati mashabiki wakisafiri umbali mrefu na wengine kulala ufukweni ili kupata nafasi ya mbele, Serikali ya Rio ilikuwa ikicheka kwa furaha kutokana na hesabu kali za kiuchumi zilizo nyuma ya tamasha hilo la bure. 

Inakadiriwa kuwa ujio wa Shakira umezalisha takribani Reali ya Brazil (BRL) milioni 777 ikiwa ni sawa na takriban Shilingi za Kitanzania bilioni 405.9. kiasi ambacho ni mara 40 ya uwekezaji uliyofanywa, huku sekta za hoteli na biashara zikichangamka vibaya mno baada ya ongezeko kubwa la wageni kutoka kila kona ya dunia. 

Usalama haukuwa wa mchezo kwani askari takribani 8,000 na mitambo ya kisasa ya utambuzi wa sura vilidhibiti hali, huku kwa mashabiki wengi, usiku huo ulikuwa ni zaidi ya burudani bali ni tamko la nguvu ya Amerika ya Kusini katika ramani ya dunia.


No comments