DHAMIRA YA SERIKALI NA UWEKEZAJI WA TRILIONI 1.2 KUIFANYA AFCON 2027 MILANGO YA FURSA TANZANIA
![]() |
| Didier Drogba akishika mkoba wa bajeti na waziri Makonda |
Serikali imedhihirisha dhamira yake ya dhati ya kuitangaza Tanzania kimataifa kwa kutenga zaidi ya Sh trilioni 1.2 katika sekta ya michezo, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuwa mwenyeji wa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2027.
Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara kwa mwaka wa fedha 2026/27, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amebainisha kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia uwekezaji huo mkubwa unaolenga timu za taifa, uendeshaji wa michezo, na miundombinu ya kisasa ili kunufaisha kila Mtanzania na fursa za mashindano hayo.
Katika kuthibitisha utayari huo, Rais Samia tayari ametoa kiasi cha Dola za Marekani milioni 30, sawa na takriban Sh bilioni 76.157, kama ada ya uandaaji wa mashindano hayo makubwa barani Afrika. Mkakati huu wa hamasa unaoratibiwa na Kamati Kuu ya Kitaifa chini ya Mwenyekiti Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, umelenga kuunganisha sekta za utalii, ukarimu, usafirishaji, na usalama ili kutoa huduma bora na kuitangaza taswira ya nchi duniani kote.
Ili kuipa mashindano haya uzito wa kipekee, serikali imeanza kushirikiana na magwiji wa soka duniani akiwemo Didier Drogba, nahodha wa zamani wa Ivory Coast na mchezaji bora wa wakati wote aliyewahi kutamba na klabu za Chelsea na Galatasaray.
Uwepo wa Drogba, ambaye pia ni mmiliki wa klabu ya Phoenix Rising ya Marekani, unatumika kama uthibitisho wa namna Tanzania inavyojipanga kutumia AFCON 2027 kuitangaza taswira yake kimataifa.
Sambamba na ushirikiano huo, serikali imeweka lengo la kukamilisha ukarabati na ujenzi wa miundombinu yote ya michezo ifikapo Agosti 2026 katika miji wenyeji ya Dar es Salaam na Arusha. Kazi katika Uwanja wa Benjamin Mkapa imefikia asilimia 95, huku viwanja vya mazoezi vya Gymkhana, Meja Jenerali Isamuhyo na Shule ya Sheria vikiwa vimekamilika tayari kwa ajili ya michuano hiyo.
Miradi mingine ya kimkakati inaendelea kwa kasi ambapo ujenzi wa uwanja mpya wa Arusha wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 32,000 umefikia asilimia 77.5, huku ujenzi wa uwanja wa Dodoma wenye uwezo wa kubeba watu 32,500 ukiwa katika hatua za awali za asilimia tano.
Aidha, serikali inaendelea na ujenzi wa Akademia ya Michezo katika Chuo cha Malya uliofikia asilimia 49, pamoja na vituo vya mazoezi na kupumzikia wananchi jijini Dodoma na Dar es Salaam vilivyofikia asilimia 73.5 na 49 mtawalia. Ukarabati wa Uwanja wa Uhuru pia unaendelea vizuri ukiwa umefikia asilimia 70, hatua inayolenga kukuza vipaji na kuboresha huduma za michezo nchini kupitia uwekezaji huu wa kihistoria uliolenga kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha michezo na utalii barani Afrika.

Post a Comment