TUME YA CHANDE YAFUNGUA NJIA YA KUSHUGHULIKIA WALA RUSHWA KUPITIA CHOMBO CHA JINAI



Mara baada ya ripoti ya Tume ya Uchunguzi wa matukio ya siku na baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2025 kuwekwa hadharani, kumeibuka hoja nzito kutoka kwa wananchi wakitaka ufafanuzi kuhusu kile wanachokiona kama ukimya wa Tume kwenye eneo la rushwa. 

Wananchi wanahoji kuwa, kwa kutilia maanani kwamba rushwa ilitajwa kuwa miongoni mwa vyanzo vikuu vilivyochochea hasira na vurugu wakati wa uchaguzi, ni kwa nini ripoti hiyo inaonekana kutokuwa na mapendekezo ya moja kwa moja ya namna ya kukabiliana na wala rushwa waliohusika kuvuruga mchakato wa kidemokrasia kwa maslahi yao binafsi. 

Hoja hizi zinabeba hisia za wananchi wanaotaka kuona hatua za haraka zikichukuliwa dhidi ya wale waliotumia fedha na madaraka yao kupotosha matakwa ya wapiga kura.

Akijibu hoja hizo kwa weledi na ufundi wa kisheria, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman, amebainisha kuwa Tume yake imegusa maeneo yote yenye viashiria vya jinai yanayohitaji uwajibikaji wa hali ya juu, ikiwemo tuhuma za rushwa kwa viongozi na wadau mbalimbali.

 Jaji Chande anafafanua kuwa, ili kuhakikisha haki inatendeka bila upendeleo, Tume imependekeza kuundwa kwa Tume ya Uchunguzi wa Kijinai kwa mujibu wa Sheria ya Tume za Uchunguzi, Sura ya 32 Toleo la 2023. Amesisitiza kuwa chombo hiki kipya hakitakuwa na kazi ya kutoa mapendekezo tu, bali kitakuwa na rungu la kisheria la kupeleleza, kufuatilia, na kuwatia hatiani wala rushwa wote kwa mujibu wa sheria za nchi iwapo itathibitika kuwa walitenda jinai hiyo.

Uchambuzi wa kina wa mapendekezo haya unaonyesha kuwa hakuna mwanya uliowachwa kwa ajili ya wala rushwa kukwepa mkono wa dola. Hatua ya kupendekeza chombo cha upelelezi wa jinai inaonyesha dhamira ya dhati ya Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kusafisha mnyororo wa uongozi na kuondoa utamaduni wa kulindana. 

Chombo hiki kitatumia mbinu za kisayansi na upelelezi wa kina kushughulikia tuhuma mahsusi zilizobainishwa katika taarifa ya Jaji Chande, hivyo kutoa majibu ya kisheria kwa kilio cha wananchi kuhusu mienendo mibovu ya viongozi waliohusika na rushwa.

Katika muktadha mpana zaidi, uundwaji wa chombo hiki cha jinai ni daraja muhimu kuelekea mchakato wa maridhiano na maandalizi ya Katiba Mpya kabla ya mwaka 2028 kama Tume ilivyoshauri. 

Kwa kushughulikia jinai za rushwa na vurugu sasa, taifa linaweka msingi imara wa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2030 ukiwa na mazingira safi ya kidemokrasia. Hii inathibitisha kuwa ripoti ya Jaji Chande si tu nyaraka ya kihistoria, bali ni ramani ya uwajibikaji ambapo hakuna mchochezi, mfadhili wa vurugu, wala mla rushwa atakayeweza kusimama mbele ya mizani ya haki pindi upelelezi wa kijinai utakapoanza kazi yake rasmi nchi nzima.

No comments