MAPINDUZI MAKUBWA SEKTA YA UCHUKUZI: RELI YA SGR KUELEKEA LIGANGA NA MCHUCHUMA KUANZA
Serikali
imetangaza hatua kubwa katika kuimarisha miundombinu ya uchukuzi nchini, ambapo
upembuzi yakinifu wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kwa urefu wa kilomita 1,000
umekamilika, ukiunganisha maeneo ya kimkakati yakiwemo matawi ya kuelekea
miradi ya Liganga na Mchuchuma
Hatua hii
inakwenda sambamba na maandalizi ya ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Njombe, ambao
kwa sasa upo katika hatua za mwisho za kuwalipa fidia wananchi watakaopisha
mradi huo ili kuruhusu ujenzi kuanza mara moja
Taarifa ya maendeleo hayo
imetolewa na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa wakati akizungumza na
waandishi wa habari mkoani Njombe.
Akizungumza kutoka katika mashamba
ya Njombe alisema maendeleo hayo ya miundombinu yanahusisha pia maboresho ya
Uwanja wa Ndege wa Songea ambao tayari umewekwa mifumo ya taa, hali inayowezesha
ndege kutua na kuruka wakati wowote, mchana na usiku, na hivyo kuchochea
shughuli za usafiri na biashara katika ukanda wa Nyanda za Juu Kusini
Katika kuimarisha usafirishaji wa mizigo mizito, ujenzi
wa Bandari ya Kisiwa Mgao mkoani Mtwara unaendelea kwa kasi kwa lengo la
kuhudumia shehena mchanganyiko (dry bulk cargo) kama vile makaa ya mawe na
saruji, jambo litakalopunguza gharama za usafirishaji kwa wawekezaji na
wafanyabiashara
Mageuzi
haya ya miundombinu yanatajwa kuwa mhimili mkuu wa mafanikio ya miradi ya
kitaifa ya kielelezo kama Liganga na Mchuchuma, kwani yatasaidia kusafirisha
tani milioni 1.1 za bidhaa za chuma na tani milioni 3 za makaa ya mawe
zitakazozalishwa kwa mwaka kuelekea kwenye masoko ya ndani na nje ya nchi
Post a Comment