Sauti Para sports watwaa ubingwa wa Ligi ya Mpira wa Miguu kwa Watu wenye Ulemavu




Timu ya Sauti Para sports kutoka jijini Dar es Salaam imeibuka mabingwa wa Ligi ya Mpira wa Miguu kwa Watu wenye Ulemavu baada ya kuifunga Black Eagle ya Arusha mabao 2-0 katika mchezo wa fainali uliopigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex Mwenge jijini Dar es Salaam. 

Ligi hiyo iliyohitimishwa kwa mafanikio makubwa baada ya kuchezwa kwa siku tatu ilishirikisha timu kumi zilizochuana katika makundi mawili, huku Black Eagle wakishika nafasi ya pili na Duce Parasports wakiibuka washindi wa tatu katika ushiriki wao wa kwanza. 

Katika tuzo za binafsi, kocha Abdul Machine wa Sauti Para sports alitwaa tuzo ya kocha bora wa mashindano, wakati Mohammed Munga wa Black Eagle akiibuka mfungaji bora baada ya kupachika mabao 19.

Akizungumza wakati wa hafla ya kufunga mashindano hayo yanayoratibiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu kwa Watu wenye Ulemavu Tanzania (TAFF) kwa udhamini wa Azam TV, Katibu Mkuu wa shirikisho hilo, Alfred Sentau, amesema mchezo huo umekuwa chachu ya matumaini kwa kuwapa fursa wachezaji kuonesha uwezo wao na kuthibitisha kuwa ulemavu si kikwazo cha kutimiza ndoto. 

Sentau alisisitiza kuwa mashindano hayo yanaonesha wazi kuwa watu wenye ulemavu wana uwezo mkubwa wa kushindana na kufanya vizuri, hivyo jamii inapaswa kuacha mtazamo hasi dhidi yao na badala yake kuwapa nafasi sawa kama watu wengine. 

Aliongeza kuwa ukuaji wa ligi hiyo kutoka klabu nne pekee wakati wa kuanzishwa kwake hadi kufikia klabu kumi kwa sasa ni ishara ya maendeleo makubwa ya mchezo huo nchini.

Lengo kuu la TAFF kwa sasa ni kuendelea kuiboresha ligi hiyo ili kuongeza ushindani na kuzalisha wachezaji bora watakaounda timu ya Taifa imara kwa ajili ya mashindano ya kimataifa. 

Sentau ametoa wito kwa wadau mbalimbali wa michezo kujitokeza kuunga mkono juhudi hizo za kuliwezesha kundi hilo la watu wenye ulemavu, akibainisha kuwa michezo ni njia bora ya kuwapa fursa za kujinufaisha kiuchumi, kujitegemea na kuchangia katika ujenzi wa taifa lenye usawa na ujumuishi kwa wote.


MWISHO


No comments