SERENGETI GIRLS YAING’OA BOTSWANA KOMBE LA DUNIA
Timu ya taifa ya soka ya wasichana chini ya miaka 17, ‘Serengeti Girls’, imeendeleza wimbi la furaha na mshikamano wa kitaifa baada ya kuiondoa Botswana katika kinyang’anyiro cha kufuzu fainali za Kombe la Dunia kwa jumla ya mabao 6-2.
Katika mchezo wa marudiano uliopigwa leo Aprili 19, kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, jijini Dar es Salaam, mabinti hao jasiri walionyesha ukomavu na uzalendo wa hali ya juu kwa kupata ushindi mnono wa mabao 3-0.
Matokeo hayo ni mwendelezo wa kazi nzuri iliyoanza ugenini katika Uwanja wa Obedi Itani Chilume, Francistown, ambapo Serengeti Girls ilichomoza na ushindi wa mabao 3-2.
Mchezo ulikuwa wa vuta ni kuvute, ambapo Serengeti Girls ililazimika kusubiri hadi kipindi cha pili kupata mabao baada ya kubanwa vilivyo na wageni katika dakika 45 za kwanza.
Hata hivyo, kutokana na mshikamano na ari ya kupambania bendera ya taifa, Bahati Steven alifungua ukurasa wa mabao dakika ya 60, kabla ya Harrier Juma kuongeza bao la pili dakika ya 84. Wakati wageni wakiamini mchezo umekwisha, Bahati alirudi tena nyavuni kwenye dakika za nyongeza na kupigilia msumari wa mwisho uliosababisha ubao kusomeka 3-0 na kuhakikisha Watanzania wanatoka uwanjani kwa tabasamu na amani.
Kwa ushindi huu, Serengeti Girls sasa inajiandaa kuvaana na Afrika Kusini katika hatua inayofuata, ambapo mshindi wa jumla kati yao atakutana na mshindi kati ya Kenya na Uganda.
Mafanikio haya ni kielelezo tosha cha kile ambacho taifa kinaweza kukifanya kinapokuwa na utulivu na umoja, huku macho yote sasa yakielekezwa nchini Morocco ambako fainali hizo za dunia zimepangwa kufanyika baadaye mwaka huu.
Watanzania kote nchini wanaaswa kuendelea kuishika kauli mbiu ya "Nchi Kwanza" kwa kuipa sapoti timu hiyo inayobeba matumaini ya mamilioni ya wananchi katika anga za kimataifa.

Post a Comment