REKODI MPYA: TRA Yakusanya Trilioni 28 Ndani ya Miezi Tisa, Yavuka Malengo kwa Kishindo
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeandika historia mpya baada ya kukusanya jumla ya Shilingi trilioni 28.005 katika kipindi cha miezi tisa (Julai 2025 – Machi 2026), ikiwa ni ongezeko la asilimia 16.5 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita.
Taarifa iliyotolewa na Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, inaonesha kuwa mamlaka hiyo imevuka lengo lake la kukusanya Shilingi trilioni 26.773 kwa ufanisi mkubwa.
Mafanikio haya yamechagizwa zaidi na utendaji wa mwezi Machi 2026 pekee, ambapo TRA imekusanya Shilingi trilioni 3.58, sawa na ufanisi wa asilimia 107.6 dhidi ya lengo la trilioni 3.32.
Katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha (Januari – Machi 2026), makusanyo yamekua kwa asilimia 23.6, yakifikia Shilingi trilioni 9.31 na kuimarisha uwiano wa kodi kwa Pato la Taifa (GDP) hadi asilimia 14.1 kutoka asilimia 13.7.
Ongezeko hili la mapato linaendana na kasi kubwa ya usajili wa walipakodi wapya. Kati ya Julai mwaka jana na Machi mwaka huu, TRA imesajili walipakodi wapya 900,755, ikivuka lengo la awali la kusajili watu 685,706 kwa asilimia 131. Hadi kufikia mwishoni mwa Machi 2026, idadi ya walipakodi waliosajiliwa nchini imefikia 8,245,704.
Mbali na makusanyo, mamlaka hiyo imeimarisha usimamizi wa haki na utatuzi wa migogoro. Ndani ya miezi mitatu iliyopita, TRA imetatua migogoro 30 nje ya mahakama yenye thamani ya Shilingi bilioni 800.8, huku ikiendelea kudhibiti ukwepaji kodi kwa kukamata mizigo ya magendo na kuokoa mabilioni ya fedha kupitia chunguzi maalum.
Katika kukuza mazingira ya biashara, TRA imetoa marejesho ya kodi (tax refunds) ya Shilingi bilioni 893.6 ili kusaidia mzunguko wa fedha kwa wafanyabiashara. Aidha, kupitia ushirikiano na Tiseza, wawekezaji wapya 139 wamesajiliwa na misamaha ya kodi yenye thamani ya Shilingi bilioni 660.8 imetolewa ili kuchochea ajira na kukuza uchumi wa viwanda nchini.

Post a Comment