RAIS SAMIA AELEKEZA MATUMIZI YA USAFIRI WA PAMOJA SERIKALINI



 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewaelekeza maafisa na watumishi wa ofisi yake kutumia usafiri wa pamoja (mabasi madogo) katika safari za kikazi. Hatua hiyo imelenga kubana matumizi ya nishati ya mafuta na gharama za uendeshaji katika kipindi hiki.

Akizungumza leo tarehe 08 Aprili, 2026 katika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma, Rais Samia amesema ameanza kutekeleza uamuzi huo upande wake kwa watendaji wanaofuatana naye. Aidha, amezitaka Wizara na Taasisi nyingine za Serikali kuchukua hatua kama hizo za kupunguza matumizi ya mafuta.

Rais amebainisha kuwa hali ya vita inayoendelea Mashariki ya Kati imeathiri nchi nyingi duniani, ikiwemo Tanzania, kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta na bidhaa. Hata hivyo, amesisitiza kuwa Tanzania bado ipo katika hali nafuu ya upatikanaji na bei ya mafuta ikilinganishwa na nchi nyingine.



Katika hatua nyingine, Rais Samia amewataka wafanyabiashara nchini kutoitumia fursa ya kupanda kwa bei ya mafuta kupandisha bei za bidhaa kiholela. Amesisitiza kuwa katazo hilo linahusu zaidi bidhaa ambazo tayari zipo maghalani ambazo hazipaswi kuathiriwa na mabadiliko ya sasa ya bei.

Amesema kuwa serikali inaendelea kufuatilia kwa karibu hali ya upatikanaji wa mafuta nchini. Pia amewahakikishia wananchi kuwa nchi ina akiba ya mafuta inayotosheleza mahitaji kwa takribani miezi mitatu ijayo.

Maelekezo hayo yametolewa wakati wa hafla ya kuwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua hivi karibuni, akiwemo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, pamoja na viongozi wengine wa Wizara na Tume ya Utumishi wa Mahakama.

No comments