Prof. Kabudi, Balozi Kombo wakutana na mjumbe wa Jumuiya ya Madola



RAIS Mstaafu wa Malawi, Mhe. Lazarus Chakwera, ambaye ni Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Mhe. Shirley Ayorkor Botchwey, amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi waandamizi wa Serikali jijini Dar es Salaam leo Aprili 9, 2026. 

Katika mfululizo wa mikutano hiyo ya kidiplomasia, Mhe. Chakwera amekutana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo.

Mikutano hiyo imefanyika mara baada ya mapokezi ya kidiplomasia ambapo Mhe. Chakwera alielekea katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) kukutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Serikali. 



Mazungumzo na Balozi Kombo yalifungua rasmi ratiba yake ya kikazi nchini inayohusisha kukutana na wadau mbalimbali wa kiserikali na kidiplomasia ili kuimarisha mahusiano na mashirikiano kati ya Tanzania na Jumuiya ya Madola.

Mhe. Chakwera aliwasili nchini Aprili 8, 2026, na kupokelewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Ngwaru Maghembe. 

Ziara hii ya kikazi inatarajiwa kuwa ndefu na yenye tija, ambapo kiongozi huyo atatembelea miji ya Dar es Salaam, Dodoma, na Zanzibar kukutana na makundi mbalimbali ya kijamii na kisiasa.

Katika ratiba yake inayotarajiwa kuhitimishwa Aprili 16, 2026, Mhe. Chakwera amepangiwa miadi ya kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Serikali, wakuu wa vyama vya siasa, wawakilishi wa asasi za kiraia, pamoja na viongozi wastaafu wa kitaifa. 

Ziara hii inasisitiza dhamira ya Jumuiya ya Madola katika kuendeleza ushirikiano wa karibu na Tanzania katika masuala ya utawala bora, maendeleo, na uthabiti wa kikanda.

No comments