NYOKA MKUBWA AUAWA NA WANANCHI KATA YA MILOLA BAADA YA KUZUA TAHARUKI NA HOFU



Nyoka mkubwa aliyekuwa akifugwa ameuawa na wananchi wa Kata ya Milola, Wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro, kwa ushirikiano na Jeshi la Polisi, baada ya kiumbe huyo kusababisha taharuki na hofu kubwa katika eneo la Mavimba. 

Tukio hilo lilitokea katika njia panda ya mnadani, ambapo uwepo wa nyoka huyo uliwaogopesha wakazi wa eneo hilo na kusababisha baadhi yao kusitisha shughuli zao za kiuchumi kwa kuhofia usalama wa maisha yao. 

Mkaguzi wa Kata ya Milola, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi (A/INSP) Aloyce Andrew, aliongoza operesheni hiyo kufuatia malalamiko ya wananchi waliokuwa na wasiwasi na madhumuni ya ufugaji wa nyoka huyo katikati ya makazi ya watu.

Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi limetoa onyo kali dhidi ya kujiingiza katika imani potofu ambazo zimekuwa zikivuruga amani, utulivu na mshikamano ndani ya jamii. 

Mkaguzi Andrew amesisitiza kuwa vitendo vinavyoambatana na imani hizo ni kikwazo kikubwa kwa maendeleo, kwani vinaleta hofu inayozorotesha juhudi za wananchi katika kujitafutia riziki. 



Amesema kuwa amani ya kweli inategemea kuheshimiana na kuepuka vitendo vinavyoweza kuleta migogoro au taharuki miongoni mwa majirani, huku akimtaka mwananchi aliyekuwa akimfuga nyoka huyo kuacha mara moja tabia hiyo inayotishia usalama wa wengine.

Katika kutilia mkazo kampeni ya kitaifa ya maridhiano na mshikamano, wananchi wamehimizwa kuendelea kushirikiana kwa karibu na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za viashiria vya uhalifu mapema. 

Ushirikiano huo unatajwa kuwa ndiyo njia pekee ya kuhakikisha kuwa amani ya nchi inalindwa na hatua za kisheria zinachukuliwa kwa wakati dhidi ya watu wanaokiuka taratibu. 

Kwa kumuua nyoka huyo, hali ya utulivu imerejea katika eneo la Mavimba, na wananchi wameshauriwa kuzingatia uzalendo na umoja ili kuendelea kuijenga Tanzania yenye usalama na amani kwa kila mmoja.

No comments