MEYA MNYONGE AHIMIZA UZALENDO NA DIPLOMASIA KWA VIJANA ASEMA HAKUNA NJIA YA MKATO




Katika kilele cha kampeni ya kitaifa ya kuimarisha amani, utulivu, na mshikamano, Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Songoro Mnyonge, ametoa mwito mzito kwa vijana kurejea katika misingi ya uzalendo kwa kutoa majibu ya kimaendeleo badala ya kulalamika. 

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa jukwaa la ‘Vijana Platform’, Meya Mnyonge amesisitiza kuwa taifa la kesho linategemea vijana ambao wako tayari kuipenda nchi yao kama wanavyopenda familia zao, huku akionya kuwa hakuna njia ya mkato ya mafanikio zaidi ya kukaa chini na kutoa hoja zenye mashiko.

Mnyonge amebainisha kuwa uzinduzi wa jukwaa hilo ndani ya wilaya ya Kinondoni ni sehemu ya mkakati wa serikali wa kuwashirikisha vijana moja kwa moja ili waweze kutoa maoni, mapendekezo, na kushirikisha changamoto zinazowakabili. 

Amesema kuwa ulimwengu wa sasa unahitaji vijana wasomi na wabunifu ambao wako tayari kutumia teknolojia na kasi ya mabadiliko kuliandalia taifa Dira ya 2050, huku akisisitiza kuwa njia pekee ya kusikika ni kupitia meza ya mazungumzo na si mihemko inayoweza kuhatarisha amani iliyopo.

Kauli ya Meya huyo imepokelewa kwa hisia tofauti mitandaoni huku, wadau wengi wa amani wakipongeza hatua hiyo ya Meya, wakisema kuwa inawatoa vijana katika hali ya kuwa watazamaji na kuwafanya washiriki hai wa maendeleo. Kauli hizi zinaakisi kiu ya jamii kuona vijana wanajengewa moyo wa kuipenda, kuilinda, na kuitumikia nchi yao kwa vitendo badala ya kujiingiza katika siasa za majitaka.

Katika kuitetea kazi inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, wafuasi wa amani wameonya dhidi ya wale wanaojaribu kupandikiza sumu ya chuki na uchochezi. 

Imeelezwa kuwa juhudi zinazofanyika sasa zinagusa maisha ya mnyonge moja kwa moja, na kila anayejaribu kuchezea misingi ya nchi kwa kisingizio cha utetezi wa wananchi anapaswa kutambua kuwa muda wa siasa za vurugu umepita. Tanzania inasonga mbele kwa vitendo, diplomasia, na mshikamano, huku vijana wakihimizwa kuchangamkia fursa na kuacha matusi ya kilevi yanayolenga kuivuruga amani na utulivu adhimu uliopo nchini kwa sasa.

No comments