KISHINDO KOMBE LA DUNIA 2026: DSTV KURUSHA MECHI ZOTE 104 KWA KISWAHILI
Na Rahel Pallangyo
Mashabiki wa soka barani Afrika wanatarajiwa kushuhudia historia mpya katika mashindano ya Kombe la Dunia 2026, baada ya Kampuni ya DStv kupitia SuperSport kuthibitisha kurusha mubashara mechi zote 104 za michuano hiyo.
Hatua hii inakuja wakati muundo wa mashindano hayo ukifanyiwa mabadiliko makubwa ambapo kwa mara ya kwanza, idadi ya timu washiriki imeongezeka kutoka 32 hadi 48, huku bara la Afrika likiweka rekodi ya kuwakilishwa na timu 10. Matangazo hayo yatakayopatikana kupitia DStv na huduma ya DStv Stream, yatatolewa kwa lugha mbalimbali ikiwemo Kiswahili, Kiingereza, na Kireno ili kukidhi mahitaji ya watazamaji wengi zaidi barani kote.
Katika kujiandaa na tukio hilo la kihistoria linalotarajiwa kuanza Juni 11, 2026, SuperSport imepanga kuleta mapinduzi katika uchambuzi wa michezo kwa kuanzisha vipindi vipya vya majarida na makala maalum.
Vipindi hivyo vitaongozwa na nyuso mpya pamoja na wataalamu wa soka waliobobea kutoka ndani na nje ya Afrika, lengo likiwa ni kutoa vionjo vya kipekee vinavyoendana na tamaduni za Kiafrika.
Sherehe za ufunguzi zitakazofanyika jijini Mexico City zitakuwa mwanzo wa safari hiyo ya mwezi mmoja itakayofika tamati Julai 19, 2026, katika jimbo la New Jersey nchini Marekani.
Mkurugenzi wa CANAL+ anayehusika na maudhui ya michezo kwa nchi zinazozungumza Kiingereza na Kireno Afrika, Rendani Ramovha, ameeleza fahari yake katika kuwafikishia Waafrika jukwaa hilo kubwa la michezo duniani.
Amesema kuwa kuwepo kwa timu nyingi za Afrika nchini Mexico, Canada, na Marekani kunatoa hamasa ya kipekee, hivyo wamejipanga kutoa huduma bora kupitia "Nyumba ya Mabingwa" ili wateja wao wasikose hata dakika moja ya matukio hayo muhimu. Timu za Afrika zitakazobeba matumaini ya bara hili ni pamoja na Senegal, Algeria, Tunisia, Misri, Ivory Coast, Ghana, Cape Verde, Afrika Kusini, DRC na Morocco.
Ongezeko la mataifa washiriki na ushiriki mpana wa timu za Kiafrika unatazamwa kama fursa adhimu ya kukuza vipaji na kueneza soka la Afrika katika ramani ya dunia.
Kwa kurusha mechi hizo kwa lugha za asili kama Kiswahili na Kizulu, DStv inalenga kuleta uhalisia na msisimko wa viwanja vya Marekani Kaskazini moja kwa moja hadi kwenye sebule za mashabiki.
Hii inatajwa kuwa ni moja ya hatua kubwa za kimkakati katika kuhakikisha kuwa soka linabaki kuwa kiunganishi kikuu cha kijamii na kiuchumi barani Afrika.
Post a Comment