JWTZ YATANGAZA NAFASI ZA KUANDIKISHWA JESHI KWA VIJANA 2026




Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limetangaza nafasi za kuandikishwa jeshini kwa vijana wa Kitanzania wenye elimu kuanzia kidato cha nne hadi elimu ya juu ambapo watakaofanikiwa watapatiwa mafunzo ya kijeshi na kuendelezwa katika taaluma zao. 

Kwa mujibu wa Taarifa kutoka JWTZ iliyosainiwa na Mkuu wa Kitengo cha Habari na Uhusiano, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Luteni Kanali Kevin Baraka Byabato waombaji wanatakiwa kuwa raia wa Tanzania wa kuzaliwa wenye umri usiozidi miaka 25 kwa waliohitimu kidato cha nne na sita, na usiozidi miaka 28 kwa wenye elimu ya juu. 

Sifa nyingine ni pamoja na kuwa na afya njema, akili timamu, tabia na nidhamu nzuri, na kutokuwa na hatia ya makosa ya jinai au kufungwa. Mwombaji awe na cheti halisi cha kuzaliwa na vyeti vya shule, huku akitakiwa kuwa hajawahi kutumikia vyombo vingine vya ulinzi na usalama kama Polisi, Magereza, au Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo.

 Aidha, ni sharti awe amehitimu mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa mkataba wa kujitolea wa miaka miwili au mujibu wa sheria na kutunukiwa cheti, ingawa vijana waliopo makambini kwa sasa hawahusiki. 

Maombi yote yaandikwe kwa mkono na yawasilishwe Makao Makuu ya Jeshi Msalato Dodoma kuanzia tarehe 15 Aprili hadi 28 Aprili, 2026 yakiambatana na nakala ya kitambulisho cha taifa au namba ya NIDA, nakala za vyeti vya kuzaliwa, shule, chuo, na JKT, pamoja na namba ya simu ya mwombaji. 

Maombi hayo yatumwe kwa Mkuu wa Utumishi Jeshini, Makao Makuu ya Jeshi, S.L.P 194 Dodoma.


No comments