DDC Kariakoa na Mapinduzi ya Ajira jijini Dar es Salaam



Serikali imeendelea kuimarisha juhudi zake za kuwezesha wananchi kiuchumi kwa kujenga miundombinu rafiki ya biashara inayochochea ajira endelevu. Hatua hii imedhihirika kupitia mradi wa Kituo cha Kitega Uchumi cha DDC Kariakoo, kilichojengwa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa gharama ya Sh bilioni 36.7.

Uwekezaji huu ni kielelezo cha utekelezaji wa sera za serikali katika kuimarisha mazingira ya kufanyia biashara. Kupitia ubunifu wa kupanua wigo wa jengo hilo kutoka kuwa na maduka 94 hadi kufikia zaidi ya maduka 1,000, Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam imefanikiwa kutengeneza fursa za ajira kwa wafanyabiashara zaidi ya 4,000. Juhudi hizi zinaondoa vikwazo vya ukosefu wa nafasi za biashara na kutoa mazingira bora yanayowawezesha wananchi kujipatia kipato na kuchangia katika pato la taifa.





Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2026, Wazo Mwang’onda, alipongeza jitihada hizo na kuwataka halmashauri nyingine nchini kuiga mfano huo wa ubunifu katika uwekezaji. Alisisitiza kuwa uwezeshaji unaotolewa na serikali kuu kwa halmashauri ndio msingi mkuu wa utekelezaji wa miradi hii mikubwa inayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja.

Katika kuendeleza ajenda ya maendeleo, Mwenge wa Uhuru ulikagua jumla ya miradi saba yenye thamani ya Sh bilioni 51.825 katika Wilaya ya Ilala. Miradi hiyo inajumuisha ujenzi wa barabara ya Lindi (kilometa 1.015) kwa kiwango cha lami, inayolenga kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na huduma, pamoja na ujenzi wa miundombinu ya maji safi iliyotekelezwa na DAWASA katika Mtaa wa Ilala Kota.

Miradi hii si tu kwamba inaongeza thamani ya maeneo husika, bali inaweka mazingira wezeshi ya kijamii na kiuchumi ambayo yanachochea ukuaji wa sekta binafsi, kupunguza msongamano, na kuboresha huduma za msingi kwa wananchi, jambo ambalo ni kipaumbele cha serikali katika kuwaletea maendeleo watu wake.

No comments