Akiwa na miaka 45 ,Mrimbwende wa Korea ,Kim Min-kyung atangaza ujauzito

 



Mwigizaji na mshindi wa zamani wa taji la Miss Korea, Kim Min-kyung, mwenye umri wa miaka 45, ametangaza habari njema ya ujauzito wake huku akielezea furaha na mshangao mkubwa kutokana na umri wake. 

Kupitia ukurasa wake wa Instagram , Kim alichapisha picha za kipimo cha ujauzito na picha ya ultrasound huku akiandika kuwa hakuwahi kufikiria kama angekuja kutangaza jambo kama hilo katika umri alionao sasa.

Alibainisha kuwa mtoto huyo ni zawadi ya thamani iliyokuja katika maisha yake, huku akiwaomba mashabiki na wafuasi wake kumuombea ili kiumbe hicho kilichopo tumboni mwake kiendelee kuwa na afya njema na kuzaliwa salama duniani.

Hatua hii inakuja baada ya Kim kufunga pingu za maisha katika sherehe za harusi zilizofanyika jijini Seoul mnamo mwezi Novemba mwaka 2024, ambapo tangu wakati huo amekuwa akishirikiana na mashabiki wake picha za maisha yake ya ndoa na harakati zake za kila siku kupitia mitandao ya kijamii. 

Kim Min-kyung, aliyezaliwa mwaka 1981, alijizolea umaarufu mkubwa nchini mwake mwaka 2001 alipotawazwa kuwa mshindi wa shindano la urembo la Miss Korea. 

Baada ya kuingia katika tasnia ya uigizaji, ameweza kung'ara katika tamthilia mbalimbali zilizopendwa zikiwemo "Letter to Parents," "The Famous Seven Princesses," "Mom's Dead Upset," "Padam Padam," na "Eve’s Love," na kuendelea kubaki kuwa mmoja wa mastaa wenye ushawishi nchini humo.


No comments