Wanahabari Waandika Historia ya Kijani Shamba la Ihefu
Katika kuadhimisha kilele cha mkutano wa asasi ya MISA TAN waandishi wa habari waliamua kuacha kalamu na karatasi kwa muda na kushika majembe ili kuweka alama ya kijani katika Shamba la Miti la Ihefu lililopo ndani ya himaya ya Msitu wa Sao Hill mkoani Iringa.
Tukio hilo lililoshuhudia upandaji wa zaidi ya miti 100 ni sehemu ya jitihada za kuimarisha shamba hilo lenye ukubwa wa hekta 17,670.53, ambalo ni mhimili muhimu wa ikolojia na uchumi wa kanda ya kusini.
Hatua hii ya wanahabari inatafsiriwa kama mwanzo wa muungano mpya kati ya sekta ya habari na wahifadhi katika kulinda rasilimali za misitu ambazo ni uti wa mgongo wa viwanda na mazingira nchini.
Upandaji wa miti hii ndani ya shamba la Ihefu una faida kubwa kimazingira na kiuchumi, kwani unasaidia kurejesha uoto wa asili na kuimarisha uwezo wa ardhi kuhimili mabadiliko ya tabianchi.
Kitaalamu, kila mti uliopandwa unachangia katika kufyonza hewa ukaa na kuzalisha hewa safi ya oksijeni, huku mizizi ya miti hiyo ikifanya kazi ya kulinda udongo usichukuliwe na maji au upepo na hivyo kulinda vyanzo vya maji vinavyotegemewa na maelfu ya wananchi.
Kiuchumi, shamba hili ni chanzo cha malighafi za mbao, karatasi na nguzo za umeme, hivyo kila mti unaopandwa leo ni uwekezaji wa fedha na ajira kwa vijana wa Kitanzania katika miaka ijayo.
Tukio hili linatoa fundisho kubwa na onyo kwa jamii kuhusu umuhimu wa kuthamini rasilimali za misitu na madhara ya uharibifu unaotokana na shughuli za kibinadamu.
Mhifadhi Mkuu wa Sao Hill, Teddy Yoramu, ameweka wazi kuwa jitihada hizi za kupanda miti zinaweza kufutika ndani ya dakika chache ikiwa jamii haitabadili mtazamo kuhusu matumizi ya moto.
Ni onyo kwa wale wanaochoma mkaa au kusafisha mashamba kwa moto bila tahadhari, kwani njiti moja ya kiberiti ina uwezo wa kuteketeza uwekezaji wa miaka 20 na kuharibu mfumo mzima wa maisha ya viumbe hai na binadamu.
Ushiriki wa waandishi wa habari katika shughuli hii ni wito kwa jamii kuelewa kuwa uhifadhi si jukumu la Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) pekee, bali ni wajibu wa kila mwananchi.
Mwenyekiti wa MISA Tanzania, Edwin Soko, amesisitiza kuwa kwa kuingia shambani, wanahabari wameonyesha mfano kuwa ni lazima tuitangaze Tanzania kwa vitendo na kulinda kile tulichonacho. Ujumbe huu unalenga kuichochea jamii kuacha utegemezi wa kupindukia wa misitu kwa ajili ya nishati ya mkaa na badala yake kuanza kupanda miti kwenye maeneo yao na kulinda misitu ya serikali kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.








Post a Comment